December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Kasilda awatahadharisha wachimbaji Madini Same

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni ametahadharisha tabia ya ukiukwaji wa Sheria uwepo wa watu walioingia kinyemela na kuanza kuchimba Madini katika eneo ambalo ni karibu na chanzo cha maji kinacho tegemewa na zaidi ya wakazi 21000 wa kata mbili Za Kisiwani na Msindo Wilayani humo.

Ametoa onyo hilo akiwa na kamati ya Usalama Wilaya ya Same wakati wa Oparesheni maalum ya kushtukiza kufuatilia taarifa za kuwepo shughuli za uchimbaji madini Aina ya Dhahabu unaofanyika kinyume na taratibu Za kisheria.

Kwa mujibu wa mkuu wa Wilaya ya Same taarifa zilizo mfikia ni kwamba mbali na wachimbaji hao kufanya shughuli zao kinyemela pia wanatumia vyanzo vya Maji ambavyo vipo karibu na machimbo hayo kusafishia madini wakitumia pia Mercury na kuhatarisha Usalama wa watumiaji wengine wa maji hayo.

“Kuingia huku kinyemela na kuharibu miundombinu ya Maji ni hujuma hatutavumilia vitendo kama hivi, niwatake Jeshi la Polisi kuweka kambi kwenye eneo hili kuimarisha ulinzi kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinakoma na waliohusika kuihujumu Serikali lazima watafutwe popote na wachukuliwe hatua”. Alisema Kasilda Mgeni mkuu wa wilaya ya Same.

Mbali na hayo amewagiza pia wataalam wa Maji kutoka Wilayani kupima Maji hayo haraka kubaini endapo yanafaa kwa matumizi ya kawaida kwa binadamu na kama yakionekana yana dosari yoyote basi Wananchi wasiyatumie na kuangalia mbadala wa chanzo kingine.

Aidha ameagiza wachimbaji wadogo ambao wanamiliki maeneo hayo ya uchimbaji kuhakikisha wanatimiza taratibu zote za kisheria za uchimbaji Madini na kuwasilisha ofisini kwake kwanza kwa ajili ya ukaguzi wa nyaraka zao kukomesha wimbi la watu kuvamia maeneo bila kufata taratibu za kisheria

Awali Mkurugezi wa Kampuni ya Same Gold Mining Elimino John Bina amemshukuru Mkuu huyo wa wilaya kwa ushirikiano wa kutosha baina yake na Serikali pamoja na wananchi wa maeneo hayo na kuahidi kushirikiana na wachimbaji wengine kudhibiti shughuli yoyote ya uchimbaji kinyume na taratibu za kisheria.

“Nakuahidi mkuu wa wilaya kuwa nitatoa ajira ya kutosha kwa vijana na kufanya shughuli za maendeleo katika kata ya msindo kijiji cha Duma na kuwa mlinzi wa maeneo hayo”. alisema Elimino John Bina Mkurugezi wa Kampuni ya Same Gold Mine.

Aidha ameshukuru pia serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya Rais wake Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuthamini wachimbaji wadogo wa Madini.