Na Esther Macha, Timesmajira,Online,Rungwe
SERIKALI wilayani Rungwe Mkoani Mbeya imetoa mwezi mmoja kwa maafisa maendeleo ya jamii na watendaji wa vijiji kuhakikisha wanapata takwimu za watu wenye ulemavu kwa kila kijiji na mtaa na kuwa idadi kamili ili serikali iweze kuwafikia na kufahamu mahitaji yao.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe , Dkt.Vicent Anney wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake juu ya mikakati ya kuwatambua walemavu na kujua changamoto zao katika wilaya hiyo.
“Juzi tuliadhimisha siku ya walemavu duniani wakati wa maadhimisho hayo tulijadili sana mahitaji yao na kilichokuwa kinakosekana ni takwimu za watu wenye ulemavu wako wapi na wanafanya nini ,kwa hiyo nilitoa maagizo kuwa ifikapo Januari mosi mwaka 2022 kuwe na takwimu kwa kila kijiji na mtaa kwa kuwa idadi ya walemavu waliopo katika wilaya ya Rungwe ili waweze kuwafikia,lakini pia nimewapa ofisi hapa kwangu ili tuweze kuwafikia kirahisi zaidi ,nilichokutana nacho hapa watu walikuwa wanaona siku ya walemavu kama kitu cha kawaida tu”amesema Mkuu huyo wa wilaya.
Aidha Dkt.Anney amesema kuwa kufuatia kuwepo kwa changamoto za watu wenye ulemavu ameahidi kukutana na walemavu kila baada ya miezi miwili ili kujadili masuala ya watu wenye ulemavu .
Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya amehaidi kutoa fimbo kumi kwa wasiiona ili ziweze kuwasaidia , na pia kuhaidi kutoa fedha zaidi ya mil.2 kwa ajili kutoa mafunzo ya lugha za alama kwa watu wenye ulemavu wa kusikia na kwamba serikali inataka kuona kuwa walemavu ni sehemu ya jamii .
Akizungumzia kuhusu kuficha watoto wenye ulemavu , Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa wana Rungwe wamebadilika sana kutokana na kupata shule kwa muda mrefu na kuona kuwa watu wenye ulemavu kwao ni kitu cha kawaida na sio laana na kwamba hata hivyo wanajitajitahidi kuwaonyesha kwa jamii na kushirikisha jamii na kuwa tofauti na maeneo mengine.
“Unajua wana Rungwe wamebadilika sana na wana utofauti sana na maeneo mengine ,hawa wamepata shule muda mrefu kwa hiyo ulemavu wanaona sio laana kwao ni jambo la kawaida wanajitahidi kuwaonyesha kwa jamii watu wenye ulemavu na ndo maana ukienda shule yetu ya Katumba ya watoto wenye mahitaji maalum utakuta kuna idadi kuwa ya watoto wengi wenye ulemavu wapo shule “amesema Dkt. Anney .
Kwa upande wake Mbunge wa vitimaalum Mkoa wa Mbeya , Suma Fyandomo amesema kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya ya Rungwe wamekuwa wakifanya jitihada za kufahamu changamoto za walemavu waliopo wilayani humo.
“Lakini mimi kwa nafasi yangu nimekuwa nikifanya ziara ya kuwatembelea watoto wenye ulemavu katika shule ya Katumba iliyopo wilayani humo katika kutatua changamoto za walemavu shuleni hapo ,huku nikiwataka watoto hao kutojitenga na watoto wengine kutokana na ulemavu walio nao bali nao wajione ni sawa na watoto wengine , unajua hii shule ipo mchanganyiko na watoto wengine na serikali ilifanya hivi kundi hili la watoto wenye lisijione tofauti na watoto wengine “amesema Mbunge Fyandomo.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua