November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC asimamisha shughuli za utafiti madini

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline, Songwe.

MKUU wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda, amesimamisha shughuli za utafiti wa madini ya dhahabu zinazofanywa na Kampuni ya Gold Valley Company Limited katika mto Zira kijiji cha Ileya kata ya Ifwenkenya, Wilayani Songwe, kutokana na kampuni hiyo kukiuka taratibu na sheria.

DC Itunda alitoa katazo hilo, Novemba 16, 2023 baada ya kufanya ziara katika eneo hilo akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo, ikiwa ni siku chache baada ya Mkuu huyo wa Wilaya kupokea ripoti ya timu ya wataalam aliyoiunda baada ya kupokea malalamiko ya wananchi juu ya uchafuzi wa maji ya mto Zira ambayo huyatumia.

Amesema kuwa,kampuni hiyo pia haikuwa na vibali kutoka NEMC na Mamlaka ya Bonde la Ziwa Rukwa na baadhi ya wananchi kulalamika wakidai kuwa maji awanayotumia yamekuwa na kemikali zinazotokana na shughuli hizo.

“Niliunda kamati ya wataalamu kwa niaba ya Kamati ya Usalama ya Wilaya na wakawasilisha ripoti, baada ya kupitia ripoti ile ilibainisha wazi kwamba kampuni ilianzisha shughuli bila kufuata taratibu za kisheria,

“Kwa kuzingatia ripoti ya timu ya wataalamu tumekuja na maamuzi yafuatayo kwanza kuanzia leo shughuli zote zinazoendelea kufanyika katika mto huu wa Zira zisimame,”ameeleza DC Itunda.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) waanze kufuatilia kuanzia walipoanza kufanya utafiti wao na wawasilishe ripoti ofisini kwake.

Kabla ya uamuzi huo, kampuni hiyo ilipewa nafasi ya kurekebisha mapungufu hayo baada ya Kamati hiyo kutembelea eneo hilo Oktoba 3 mwaka huu, lakini hadi kufikia Novemba 16 ilikuwa haijatekeleza maagizo hayo.

DC Itunda ameeleza kuwa Serikali inawapenda wawekezaji lakini wanaofwata taratibu hivyo ameuagiza uongozi wa kampuni hiyo kukamilisha maagizo ili iweze kuendwlea na shughuli zake.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni hiyo, Amani Msumba amesema kuwa wamepokea maagizo hayo huku akiahidi kuwa watayafanyia kazi.

“Nashukuru sana kwa ujio wa Mkuu wa Wilaya na maagizo aliyotuachia,Kwa niaba ya kampuni tutatekeleza yote aliyotuagiza na tutafwata taratibu na zitakapokuwa zimekamilika tutawasiliana naye ili kuendelea na shughuli kama kawaida” alieleza mwakilishi huyo kwa kifupi.

Diwani wa Kata ya Infwenkenya, Pius Omboka amesema kuwa pamoja na kampuni hiyo kutokamilisha taratibu lakini ilikubaliana na wananchi wa eneo hilo kabla ya kuanza shughuli hiyo.