Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online. Shinyanga
WATUMISHI wa Serikali Wilaya na Mkoa wa Shinyanga, wametakiwa kujiepusha na kulipana posho kwa ajili ya vikao vya maandalizi na mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, utakapokuwa wilayani Shinyanga.
Agizo hilo limetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko ambapo amesema hakuna sehemu yoyote ndani ya sheria inapoelekezwa mtumishi kulipwa posho kwa ajili ya maandalizi, mapokezi au kukimbiza Mwenge wa Uhuru.
Mboneko ametoa agizo hilo katika kikao cha maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kuingia katika wilaya hiyo Julai 11 mwaka huu, ambapo alisema idara yoyote ambayo watu wake watabainika kulipana posho kwa ajili ya Mbio za Mwenge wa Uhuru watakiona cha moto.
“Hakuna sehemu yoyote inayoelekeza mtumishi kulipwa posho kwenye shughuli za maandalizi, mapokezi na Mbio za Mwenge wa Uhuru, haipo, Mwenge wa Uhuru ni uzalendo, Mwenge wa Uhuru ni wetu, hakuna mtu analipwa posho kwa ajili ya shughuli za Mwenge wa Uhuru, hiyo haipo.
“Ndiyo maana tukasema tushirikiane kwenye uhamasishaji, viongozi wangu wa chama kwenye kata zote utakapopita, uhamasishaji wa wana CCM, wananchi wa kawaida wote washiriki, vyama vyote washiriki, viongozi wa dini washiriki, kila mmoja ashiriki, hakuna kulipana posho, Mwenge huu ni wetu sote, huko nyuma mlikuwa mkivuruga vuruga,” amesema.
Amesema hatokubali kupitisha matumizi yoyote ambayo ataona ndani yake, kuna kulipana posho kwa ajili ya watumishi shughuli itakuwa kubwa na atakuwa mkali kuliko pilipili ya mwendokasi, ambapo alielekeza fedha zote zitakazokusanywa zielekezwe kwenye matumizi ya vyakula, maji ya kunywa na mapambo na kwamba agizo hilo pia linawahusu madiwani ambao aliahidi kuwaeleza.
Awali katika taarifa yake kwa Mkuu wa Wilaya kuhusu miradi iliyopangwa kutembelewa, kuwekewa mawe ya msingi na mingine kufunguliwa Mratibu wa Mbio za Mwenge Kiwilaya, Charles Luchagula amesema miradi yote itagharimu sh. milioni 702.
Miongoni mwa miradi itakayotembelewa, kukaguliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu ni ujenzi wa maabara katika Shule ya Sekondari Mwalukwa yenye thamani ya sh. milioni 59, mradi wa Zahanati ya Bushushu ambapo patakwekwa jiwe la msingi na kukabidhi pikipiki tano za bodaboda kwa kikundi cha vijana Mnarani Kata ya Kitangili.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea