January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC ahimiza viongozi kuunga mkono juhudi za Rais Samia

Na Damian Kunambi, Timesmajiraonline,Njombe

WATENDAJI pamoja na madiwani wametakiwa kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kumtua mama ndoo kichwani kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo yao.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Victoria Mwanziva, mwisho mwa wiki kwenye jukwaa la wadau wa maji lililofanyika wilayani humo na kuhusisha Kamati ya Usalama, Kamati ya Siasa ya CCM ,madiwani, maofisa Tarafa, watendaji kata pamoja na timu ya wataalamu (CMT)

“Rais amefanya kazi kubwa sana wilayani kwetu kwani kwa sasa tuna miradi saba ya maji yenye thamani ya zaidi ya sh. Bilioni 13.8 ambayo inaendelea kutekelezwa, hivyo viongozi wa ngazi zote tunapaswa kusimamia fedha hizi ili zitumike ipasavyo na kuhakikisha miradi inatoa huduma stahiki”. Amesema Mwanziva na kuongeza;

“Viongozi wa ngazi zote tunapaswa kusimamia fedha hizi ili zitumike ipasavyo na kuhakikisha miradi inatoa huduma stahiki”. Amesema Mwanziva.

Aliongeza kuwa jukwaa hilo limeandaliwa madhubuti ili kujadili na kuhoji changamoto zilizopo katika miradi mbalimbali na kuweza kuzitatua ili kuwaondolea wananchi changamoto zinazowapelekea kutembea umbali mrefu kufuata maji.

Aliongeza kuwa kuna haja ya kuboresha uunganishaji wa vyombo vya utoaji huduma za maji ngazi ya jamii (CBWSO) ili kuwezesha RUWASA kukidhi vigezo vya upataji fedha kiasi cha sh. 50,000 kwa kila mtu ambaye atapata ufikiwaji wa chanzo kilichoboreshwa ikiwemo ujenzi mpya, upanuzi au ukarabati wa skimu ya maji ambapo kwa sasa wilaya hiyo bado haijakidhi vigezo vya upataji fedha hiyo.

Naye Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Jeremiah Maduhu, alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa imepokea sh. Bilioni 1.30 kwa ajili ya uchimbaji visima vya maji na kukamilisha baadhi ya miradi iliyokwama ili kuwezesha wananchi kupata maji ya uhakika na yaliyo safi na salama.

Amesema kwa mujibu wa maelekezo ua Serikali yaliyotokana na bajeti ya fedha ya mwaka 2024/2025 yameelekeza kuwa sh. milioni 300 zitatumika katika uchimbaji wa visima na millioni 700 zitatumika kukamilishhuua baadhi ya miradi ambayo yote kwa pamoja inatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 30, mwaka huu.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Wise Mgina aliwasihi madiwani wenzake kuweka usimamizi mzuri ili kuweza kupata fedha hizo kwani vijiji zaidi ya 60 vinapata maji na vinakidhi baadhi ya vigezo.

” Viongozi tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunasimamia uundwaji wa vikundi vilivyokidhi vigezo ikiwemo miradi kutekelezwa kwa ufasaha ili na sisi tuweze kupata hizo fedha ambazo zitatusaidia kuongeza wingi wa miradi ya maji,” alisema.

Hata hivyo kwa upande wao madiwani na watendaji mbalimbali wa kata walilipokea vyema suala hili huku wakitoa mawazo mbalimbali yanayoweza kuboresha miradi hiyo.