Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Kigoma
MKUU wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli ameelezea umuhimu wa vijana nchini kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) huku akionesha kukerwa na watu wasiolitakia mema Jeshi hilo kwa kusambaza taarifa za uongo kwamba mafunzo hayo yamefutwa.
Akizungumza wakati wa sherehe za kufunga mafunzo ya awali ya kijeshi oparesheni miaka 60 ya JKT kwa vijana wa Kikosi cha Jeshi 821 Bulombora JKT ,Kalli amesema kuwa Jeshi hilo limekuwa likifundisha vijana uzalendo kwa lengo la kuwafanya walipende Taifa lao lakini pia limekuwa likiwafundisha katika suala zima la stadi za maisha.
“Shukrani kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Kwa kuendeleza mafunzo haya ya kuwajengea vijana uzalendo wa kuwa na uchungu na nchi yao ,lakini wapo watu wanaosema kwamba mafunzo ya JKT yamefutwa ,watu hawa tunawalaani , hatuwapi nafasi maana jeshi hili ni muhimu kwa vijana.”amesema Kalli
Ametumia nafasi hiyo kuwataka vijana kuwa wazalendo, waadilifu katika kuilinda nchi yao badala ya kuwaachia watu wengine lakini pia wasimamie yale waliyofunza na kuyaishi huku akiwataka kutojiingiza kwenye makundi ya uhalifu kwani sasa wao ni kielelezo kwa wengine.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajab Mebele,Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amewataka vijana hao wajiepushe na vitendo vya uvunjifu wa amani ,ulevi,utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na utumiaji wa vinywaji vyenye kuhatarisha afya zao.
“Nendeni mkalitumikie Taifa kwa Juhudi na weledi ,ni vyema kila mmoja kwanza akajiuliza atalifanyia nini Taifa kabla ya kujiuliza Taifa limemfanyia nini .”alisema Brigedia Jenerali Mabena
 Aidha amesema baada ya vijana hao kumaliza mafunzo ya awali ya kijeshi kwa kipindi cha miezi minne sasa wanakwenda kuanza mafunzo ya stadi za kazi na stadi za maisha kwa kipindi cha miezi 20 kwa lengo la kuwapatia ujuzi mbalimbali ili kuwawezesha kujiajiri wenyewe mara baada ya kumaliza mkataba wao ndani ya JKT.
Kamanda Kikosi cha Jeshi 821 Bulombora JKT Luteni Kanali Juma Hongo amesema katika kipindi cha miezi minne vijana hao wamefundishwa mambo mengi ambayo yote kwa pamoja yanalenga kumsaidia kijana kuwa mzalendo lakini pia kumwezesha kujiajiri mwenyewe.
Naye mmoja wa vijana waliohitimu mafunzo hayo Cymfia Mtengwa alilishukuru Jeshi la Kujenga Taifa kwa mafunzo waliyopata ambapo amesema yatawasaidia kujiajiri kutokana na stadi walizojifunza Kikosini hapo.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba