June 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dawson: Uzimwaji wa mtandao utaleta hasara kwa nchi na wananchi wake

Na Mwandishi wetu,TimesMajira

IMEELEZWA kuwa uzimwaji wa mitandao inaweza kusababisha hasara kubwa kwa nchi na wananchi wake kutokana na baadhi ya watu kutegemea mitandao hiyo kupata ajira na ufanyaji wa biashara.

Akizungumza mwishoni mwa wiki Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki Binadamu na Utawala wa Kisheria wa Taasisi ya Reach Out Tanzania,Kumbusho Dawson wakati wa mazungumzo ya pamoja kati Asasi za Kiraia,Watetezi wa Haki za Binadamu pamoja na Waandishi wa habari.

Amesema uwepo wa mitandao unaendana na ukuaji wa teknolojia katika dunia ya sasa hivyo endapo itazimwa itakuwa imekiukwa haki za binadamu ambazo zipo kikatiba.

”Tumekutana leo hapa kujifunza,kuzungumza na kushauriana juu ya kuzuia au kusema hapana uzimaji wa mitandao ya kijamii nchini,”amesema na kuongeza

”Mtandao unapozimwa unaharibu uchumi wa watu wengi ikiwemo watu kukosa ajira,kutofanya biashara zao mfano watu wa Bolt na wanafunzi kushindwa kujisomea kwa kutafuta material,”amesema.

Amesema kama nchi inapoelekea katika uchaguzi ni vema kuhakikisha mtandao wa kijamii inaendelea kuwaka na sio kuzimwa na kufanya jamii kushindwa kujua kinachoendelea.

Dawson amesema uzimwaji wa mtandao unakiuka katiba ya nchi ibara ya 18 inazungumzia haki mbalimbali ikiwemo haki ya kupata taarifa na haki ya kuzungumza na haki ya kujumuika.

Kwa upande wake Mwanasheria kutoka Lawdowns Consult,A lphonce Lusako amesema wao kama wanasheria wamegundua kuwa uzimwaji wa mtandao uliofanyika mwaka 2020 kipindi cha uchaguzi ulivunja sheria za nchi na katiba.

”Ukisoma katiba inatoa uhuru wa mtu kutoa maoni,kutafuta taarifa,kutoa taarifa na vilevile uhuru wa kukutanika,sasa mtandao ulipozimwa kipindi kile cha uchaguzi zilivunjwa,”amesema.

Amesema katika dunia ya sasa mtandao ni sehemu ya binadamu ambapo umoja wa mataifa mwaka 2018 imetambua haki ya mtandao ni haki za binadamu, pia kuna African Declaration on Internet right ni sehemu ya binadamu hivyo uzimwaji wa mtandao 2020 ulivunja sheria za ndani,Katiba ya nchi ya Tanzania na mikataba ya kikanda na umoja wa kimataifa.

Naye Mmoja wa wadau wa Global Member Advasory Board Gendem,Dorcas Francis amesema mtandao unapozimwa kuna madhara mengi yanaweza kujitokea hususan watu kukosa taarifa kwa ufasaha kuhusu masuala mbalimbali.

Amesema kuzimwa mtandao ni kinyume cha sheria na katiba hususan kipindi cha uchaguzi kwani watu watashindwa kupata elimu ya mpigakura,taarifa mbalimbali zinazotelewa na serikali na kufanya watu kukosa taarifa hizo ambapo ni haki zao.