December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Daraja jipya Wami kukamilika Septemba

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online, Pwani

MENEJA wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani, Mhandisi Yudas Msangi, amesema Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 3.8 linalounganisha miji ya Chalinze – Pwani na Segera – Tanga litakamilika mwezi Septemba mwaka huu.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani, Mhandisi Yudas Msangi, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, mpango kazi wa ujenzi wa Daraja jipya la Wami unaoendelea mkoani Pwani.

Mhandisi Msangi amemueleza Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, mkoani Pwani wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi huo uliofikia asilimia 50.5 na kumuahidi kuwa kazi itakamilika kama ilivyopangwa.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo,Naibu Waziri Waitara amesema ujenzi wa daraja jipya la Wami ni mkakati wa Serikali katika kuongeza ufanisi katika barabara ya Chalinze – Segera na kupunguza adha kwa abiria na wasafirishaji wanaotumia daraja la zamani lenye urefu wa mita 88.75.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani, Mhandisi Yudas Msangi, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, nguzo nne za Daraja jipya la Wami ambao ujenzi wake umekamilika, mkoani Pwani.

“Kutokana na umuhimu wa daraja hili Serikali imeamua kujenga daraja jipya ili kuondoa adha katika daraja la zamani lililojengwa mwaka 1959 kutokana na kutokidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa sasa, kuwa jembamba na lenye njia moja na barabara zake unganishi kupita katika miinuko mikali na kona mbaya na hivyo kusababisha ajali za mara kwa mara”, amesema Naibu Waziri huyo.

Naibu Waziri Waitara, amemtaka Mkandarasi Power Construction Corporation ya China, Msimamzi wa mradi Intercontinetal Consultants and Tecnocrtrats Pvt ya India kwa kushirikiana na Apex Engineering Co. ya Tanzania na Meneja wa TANROADS Mkoa kuongeza vifaa na wafanyakazi ili kazi ikamilike kama ilivyopangwa na kusisitiza kwamba Serikali itaendelea kumlipa mkandarasi kwa wakati.

Aidha amewataka wafanyakazi wanaojenga daraja hilo kufanya kazi kwa uzalendo, bidii na kujifunza ili kuwezesha Taifa kuwa na wataalam wake wa madaraja makubwa siku zijazo.

Muonekano wa baadhi ya nguzo za daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 ambazo ujenzi wake unaendelea mkoani Pwani. Daraja hilo linaunganisha miji ya Chalinze – Pwani na Segera – Tanga na ujenzi wake utakamilika mwezi Septemba mwaka huu.

“Zaidi ya wafanyakazi 280 kati ya 300 wanaojenga daraja hilo ni watanzania, hivyo hakikisheni wingi wenu mnautumia kubaki na ujuzi na kufanya kazi kwa uzalendo”, amesisitiza Naibu Waziri Waitara.

Zaidi ya shilingi bilioni 67 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 ambalo limezingatia sehemu ya barabara za magari, watembea kwa miguu na vizuizi kwa ajili ya usalama hivyo linatarajiwa kupunguza ajali katika eneo la Mto Wami na kuhuisha huduma za usafiri na uchukuzi katika barabara kuu ya Chalinze – Segera.