January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Daktari Biteko azindua zahanati ya kisasa Bungoni Mtaa Mafuriko

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini Dkt.Doto Biteko ,amezindua Zahanati ya kisasa mtaa wa Mafuriko Ilala Bungoni wilayani Ilala, na kuwataka wananchi kutumia fursa ya uwepo wa zahanati hiyo kutumia huduma badala ya kwenda vituo vya afya vya mbali kufuata huduma za afya.

Akizungumza Mtaa wa Mafuriko Ilala Bungoni Dkt .Biteko aliwataka viongozi waliopewa dhamana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwakikisha wanahudumia kwa vitendo wananchi na kuinua hali za wanyonge kwa kuwapatia huduma bora wanazostahiri .

“Nawaomba wananchi wa jimbo la Ilala mumpe ushirikiano mbunge wa jimbo hili Mussa Zungu ,kwa vitendo na kumpongeza kwa kazi kubwa anayofanya ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake na kuwataka wananchi wengine waige mfano wa Mbunge Mussa Zungu .

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko alikemea watendaji wachache wanaojificha kwenye kivuli cha utaratibu wa kuchelewesha maendeleo ya wananchi ambapo aliwataka waache badala yake waendelee kuchapa kazi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kutatua kero, za wananchi na kusogeza huduma za kijamii.

Ujenzi wa zahanati ya kisasa Bungoni Mtaa Mafuriko ulianza February mwaka huu kwa jitihada za wananchi baadae Serikali ambapo zimegharimu kiasi cha shilingi milioni 351ukihusisha gharama za ujenzi, Samani,dawa na vifaa tiba na kufadhiliwa na Afrika Relief Agency na Taasisi ya Rahma International kutoka Kuwait.

Wakati wa uzinduzi wa jengo hilo Dkt. BITEKO alipata fursa ya kutembelea jengo hilo llinalojihushisha na wagonjwa wa nje OPD kliniki ya Mama na Mtoto pamoja na jengo la kujifungulia .

Akizungungumza wakati wa hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo la Ilala na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Mussa Azan Zungu amewataka watendaji kuhakikisha wanatumia vyema fursa za wafadhili wanaokuja kuwekeza kwenye sekta ya Afya na kuondoa mikwamo inayoweza kuchelewesha maendeleo.

Amesema, wilaya ya Ilala inapokea wageni wengi kwa siku, sambamba na wananchi wenye mahitaji kwenye Sekta ya Afya hivyo uwepo wa vituo hivi utasaidia kuboresha utoaji wa huduma.

Awali, akitoa taarifa ya mafanikio ya Idara ya Afya kwa . Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji Dkt. Zaituni Hamza amesema kuwa, wamefanikiwa kujenga jumla ya vituo vipya saba vya kutolea huduma na kupandisha hadhi zahanati tano kuwa vituo vya Afya, hivyo kufanya jumla ya vituo vya Afya kuwa 12.

Aliongeza kuwa kuelekea mwaka wa 2025, imekuja na miradi ya kimkakati ikiwemo uanzishwaji wa Chuo cha Afya cha Kati na Sayansi Shirikishi hospitali ya wilaya ya Kivule ambapo jengo la kwanza tayari limeshapauliwa, lengo ni kuunga mkono azma na dhamira ya Mheshimiwa Rais kuwaletea maendeleo karibu wananchi wake.

Aidha, Dkt. Zaituni alimshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuongeza bajeti kwa Wizara ya Afya hususan upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka asilimia 90.1 hadi kufikia asilimia 94 na kumuahidi Mheshimiwa Rais kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa wananchi.