Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kimepokea taarifa ya kifo cha Profesa Mwesiga Baregu kwa mshtuko na huzuni kubwa kwani pamoja na yeye kuwa mwanasiasa na mhadhiri mwandamizi katika vyuo mbalimbali hapa nchini, lakini pia marehemu alikuwa ni mwana mageuzi, muumini wa ujenzi wa demokrasia ya kweli akiamini kwa vitendo katika ujenzi wa mifumo ya kitaasisi na utawala bora.
Akizungumza na TimesMajira Online, Mwenyekiti wa Chama cha CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa, pamoja na mambo mengine Profesa Baregu alijitoa kwa dhati katika mageuzi ya Taifa katika kupata katiba mpya inayotokana na maoni ya Watanzania.
Profesa Lipumba amesema kuwa, mchango wake utakumbukwa akiwa mjumbe katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, lakini pia marehemu alishauri na kusimamia upatikanaji wa maoni ya Watanzania kwa nia ya kupata Rasimu ya Katiba iliyokidhi haja na mahitaji ya wakati wa sasa.
“Taifa limempoteza msomi mzalendo, Watanzania wamempoteza mtetezi. Wanataaluma wamempoteza mwana majumui wa Africa, wanasiasa tumempoteza mwanamageuzi wa kweli aliyeishi misimamo yake bila ya kutetereka,”amebainisha Profesa Lipumba.
Aidha, Profesa Lipumba ameongeza kuwa, CUF wanatoa rambirambi, “na pole zetu za dhati tunazituma kwa familia ya Prof.Baregu, ndugu, familia ya wana Chadema, Watanzania kwa ujumla pamoja na familia ya wanamajumui wa Afrika kwa kumpoteza nguli wa siasa na mzalendo wa kweli aliyeamini kuwa taaluma haiwezi kutenganishwa na siasa, kwani wanataaluma ndio daraja la kuunganisha tafiti na maendeleo na kufanya siasa iwatumikie wanyonge Watanzania, badala ya wanyonge kuwatumikia wanasiasa,”amesema.
“Tarehe 13 Juni nilipokea kwa masikitiko na huzuni kubwa, taarifa ya kifo cha ndugu yangu Prof. Mwesiga Baregu ambaye alikuwa Mwanazuoni mahiri na mwanachama mwandamizi wa Chama cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA),”amesema Profesa Lipumba.
Akizungumzia namba alivyofahamiana na Profesa Baregu, Profesa Lipumba amesema, alifahamiana naye vizuri wakati alipokwenda Chuo Kikuu cha Stanford mwanzoni mwa miaka ya 1980 kusomea shahada ya Uzamili katika Idara ya Sayansi ya Siasa.
“Mimi nilikuwa nimetangulia kwenye Chuo hicho nikimalizia kufanya Shahada ya Uzamili katika Maendeleo ya Uchumi. Nikiwa Chuo Kikuu cha Stanford, kabla ya Prof. Baregu kujiunga na Chuo,”amesema Profesa Lipumba.
Ameongeza kuwa, walianzisha Umoja wa Wanafunzi wa Kiafrika katika Chuo hicho walioupa jina la Stanford African Students Association kwa kifupi-SASA, “nilipendekeza jina hilo kwa maksudi kwa lengo la kusisitiza kuwa SASA ni wakati wa Afrika kuungana na kujikomboa, “.
Profesa Lipumba amesema kuwa, wanafunzi wengi wa Kiafrika Chuo Kikuu cha Stanford walitokea Afrika Magharibi, lakini alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa SASA kwa sababu ya sifa ya Tanzania kuongoza mapambano ya Ukombozi wa Bara la Afrika.
Amesema, baada ya kumaliza kipindi chake, Prof. Baregu alichaguliwa kuwa Rais wa Pili wa SASA na wanachama wa SASA walijadili matatizo ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambapo mara nyingi walikutana nyumbani kwa Prof. Baregu kufanya mijadala hiyo.
“Alikuwa hodari wa kujenga hoja juu ya umuhimu wa nchi za Kiafrika kuungana ili kupambana na ubeberu.Tukiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, miaka 1980 tulishiriki katika mijadala ya mageuzi ya uchumi yaliyokuwa yakifanyika Arts Lecture Theatre wakati mimi nilipendekeza kufanya mabadiliko kuelekea uchumi wa soko, Prof. Baregu alipinga vikali sera hizo kuwa ni za kukumbatia ubeberu, “amesisitiza Profesa Lipumba.
More Stories
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi