January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CPA.Makalla:Wananchi ondoeni dhana ya CCM kushinda kwa kubebwa

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla  amewataka wananchi kuondokana na dhana ya kuona ushindi kwa chama tawala kuwa siyo Demokrasia bali ni kubebwa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi ndogo za CCM Lumumba zilizopo Jijini Dar es Salaam, CPA. Makalla amesema, ushindi wa vyama vyote unatokana na wingi wa kura za wananchi na kudai kuwa, CCM imeshinda kwa kishindo kutokana na kuaminiwa na wananchi.

Amesema, uhalali wa ushindi wao  umetokana na wananchi kwa kazi nzuri ambayo chama hicho imekuwa ikifanya hususani katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na utatuzi wa kero kwa wananchi wake.

Pia amesema, CCM inatambua kuwepo kwa changamoto katika uchaguzi huu uliopota wa Serikali za Mitaa, hivyo amewasisitiza viongozi wa vyama vyote vya siasa kushirikiana ili waweze kutatua changamoto hizi zisijirudie katika chaguzi zijazo.

“Tunatambua kwamba zipo changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika uchaguzi huu lakini tushirikiane vyama vya siasa ambao ni wadau kuhakikisha na sisi tunakuwa sehemu ya kutatua changamoto hizo hususani katika wakati wa uteuzi wa wagombea.

Tujikite katika kutoa elimu kwa wagombea wetu hususani katika ujazaji wa fomu kila mmoja kujaza fomu kwa umakini na usahihi na kufanya hivyo kutaondoa sintofahamu kwa wahusika”, amesema CPA. Makalla.