Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online Dar.
KATIBU wa NEC, Siasa, itikadi, Uenezi na mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla, ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha CCM Mkoa wa Dar es Salaam, amewataka Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi kuendelea na utaratibu wa kutenga muda wa kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi, huku akieleza kuwa Chama cha CCM kipo kwa ajili ya kuwatatulia kero wananchi wake na si kujitenga nazo.
Makalla ameyasema hayo leo, Julai 6, 2024 katika mkutano wa viongozi wa ngazi zote na wanachama wa CCM, uliofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Makalla amesema ni vyema kila kiongozi akatambua wajibu wake katika nafasi aliyopo, ikiwa pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa kutenga muda husika katika Ofisi zao.
” CCM ni chama kinachosikiliza na kutatua kero za wananchi na si chama kinachokimbia kero za wananchi wake, hivyo nipende kuwasisitizia viongozi wote kila mmoja kwa nafasi yake kuendelea kutenga muda wa kusikiliza na kutatua kero zao na huo ndiyo uhai wa Chama chetu”. Amesema Makalla.
Pia, Makalla amewataka viongozi hao hususani wa chama cha CCM, kuwa na upendo na umoja na si kujigawa kwa makundi, huku akidai kuwa kufanya hivyo ni ishara mbaya ya uhai wa Chama.
Aidha, amewataka viongozi katika nafasi mbalimbali, kuacha kupanga safu ya wagombea uongozi katika ngazi za Mitaa, Kata na Wilaya wasiyokuwa na vigezo na kusema kuwa Chama ni Cha wana CCM na si mtu mmoja.
“Ni vyema tukawa na umoja na mshikamano na kutokuwa na makundi, lakini pia tuache kuwa na visasi..unakuta mtu tangu anagombea nafasi fulani hadi amechagulia na mpaka sasa kwa mfano ni diwani bado anaendeleza kisasi kwa kuwatafuta wale walikuwa wanampinga, hiyi siyo Demokrasia kwani kupingwa pia ni demokrasia hivyo baada ya kuchaguliwa unapaswa kuachana na yote na kufanya kazi na watu wote”, amesema Makalla.
Nae Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtenvu, amemuhakikishia CPA Makalla, ushindi wa kishindo katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa kupata kura nyingi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkubwa mwakani.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato