January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CPA Makalla awataka watendaji mpaka wa Namanga kuongeza ufanisi wa utendaji kazi

Na Agnes Alcardo, TimesmajiraOnline. Arusha

KATIBU wa NEC,Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa, CPA Amos Makalla, amewaelekeza watendaji katika kituo kilichopo katika mpaka wa Namanga’One Stop Border POST’kuongeza ufanisi wa kazi ili kuondoa vikwazo vya kibiashara

CPA Makalla ametoa agizo hilo leo Septemba 5,2024 wakati alipotembelea katika kituo hicho kilichopo katika mpaka wa Tanzania na Kenya, ili kujionea hali ya utoaji wa huduma ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Arusha ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025, uhai wa Chama, kusikiliza na kutatua kero za wananchi na maandalizi kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Aidha CPA Makalla ametoa rai kwa watendaji hao kuhakikisha wanaondoa urasimu pamoja na foleni ya malori yanayosafirisha bidhaa kwenda nchi jirani pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Taasisi mbalimbali zinatumia kituo hicho,ili kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Katika hatua nyingine CPA Makalla, amewaasa watendaji hao kudumisha mahusiano mazuri kwa sababu nchi ya Tanzania na Kenya ni nchi zinazotegemeana lakini pia ni nchi za wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Nimefurahi kusikia kwamba Tanzania tunanufaika na kituo hiki na ili tuendelee kunufaika zaidi tunatakiwa kuimarisha mahusiano katika ua nchi hizi mbili pamoja na wateja tunaowahudumia katika kituo hiki wakiwemo wasafirishaji na wasafiri”.

Awali Mkuu wa wilaya ya Longido, Ally Kali amesema maagizo yote yaliyotolewa na CPA Makalla atasimamia yafanyiwe kazi ili kituo hicho kiendelee kutoa huduma bora kwa wasafiri na wasafirishaji.

Ofisa mfawidhi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika forodha katika kituo hicho, Abdallah Mambi amesema huduma katika kituo hicho zinaendelea kuimarika siku hadi siku ambapo kwa sasa changamoto kubwa ya malori kukaa kwa muda mrefu katika kituo hicho inaendelea kupungua ambapo kwa sasa wanasafirisha bidhaa mbalimbali zikiwemo za mbogamboga, nafaka na bidhaa za pamba ikiwepo ‘Pampers’.