November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CPA Makalla ataka Barabara za Mitaa Mwanza/ Kigoma Ilala kukamilika kwa wakati

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, amemtaka Mkandarasi anayejenga Barabara za Mitaa ya Mwanza na Kigoma, kuongeza kasi ili ziweze kukamilika kwa wakati, ikiwa ni barabara mbili kati ya 20 katika Wilaya ya Ilala, ambazo zimetengeea bilioni 30 hadi ukamilikaji wake.

Makalla amesema, barabara hizo ambazo zinajengwa kwa kiwango cha lami, mifereji na taa za barabarani zinaendelea kupendezesha Jiji la Dar es Salaam ikiwa pamoja na kuwarahisishia wananchi kufika maeneo mbalimbali kwa wakati.

” Kama wenyewe mnavyoona, fedha nyingi zimeletwa katika Wilaya hii ili kuweza kukamilisha ujenzi wa barabara za Mitaa kwa kiwango cha lami, pongezi nyingi ziende kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Kuendelea kutuletea maendeleo katika Mitaa yetu”, amesema Makalla.

Awali, akikagua ujenzi wa ghorofa ya shule ya Sekondari Mnazi mmoja yenye madarasa 20, ambayo hadi kukamilika kwake itagharimi kiasi cha Sh. Bil 1.8, ameitaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kukamilisha ujenzi wa ghorofa hilo kutokana na kukaa muda mrefu bila kukamilika.

” Niendelee kutoa pongezi zangu kwa maendeleo haya mnayoendelea kuwaletea wana Ilala, kutokana na ujenzi wa ghorofa hii kutokamilika kwa muda mrefu, nikuombe Mkurugenzi wa Jiji ufanye jitihada ili uweze kukamilika kwa wakati ili wanafunzi hawa waweze kunufaika na ujenzi wa jengo hili”, ameongeza Makalla.

Nae Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura amemuondoa hofu Mwenezi Makalla kuwa watatekeleza kile alichowaagiza na kudai kuwa, miradi mingi imekuwa ikichelewa kutokana na Wakandarasi wengi kuwa na mitaji hafifu.

“Kinachosababisha mradi huu kukwama ni certificate ni Mil. 150 laiti kama Mkandarasi angekuwa na mtaji mkubwa mradi huu usingesimama, hivyo nikuombee Mh. Mwenezi kuyafanyia kazi yale maelekezo yako”, amesema Satura.