Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar
KATIBU wa NEC, Siasa, itikadi, Uenezi na mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla, ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha CCM Mkoa wa Dar es Salaam, amewaomba wananchi kukipatia Chama cha Mapinduzi (CCM) ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025.
Makalla ameyasema hayo leo Julai 8, 2024, Jijini Dar es Salaam, alipotembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Jimbo la Segerea Wilaya ya Ilala, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku saba katika Mkoa wa Dar es Salaam, ziara yenye lengo la kuangalia uhai wa Chama na utekelezwaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025.
Akizungumza na baadhi ya wagonjwa waliofika katika Kituo cha Afya cha Kinyerezi, ambapo alifika kwa ajili ya kukagua ukamilikaji wa kituo hicho kipya Cha afya, amewaomba kuendelea kukiamini chama cha CCM kwani kipo kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
” Pole na hongereni sana kwa kupata kituo hiki kipya Cha afya, haya ni maendeleo yanayoonekana na yasiyohitaji tochi kuweza kuyaona, unaweza kusimamia mwenyewe hapa katikati na kuangalia utofauti uliopo kwani mwanzo hii ilikuwa ni Zahanati na hivi sasa imepanda hadhi na kuwa kituo cha afya, haya ni maendeleo makubwa na tunaomba muendelee kukiamini Chama cha CCM na kukupa ushindi wa kishindo katika chaguzi zijazo”, amesema Makalla.
Aidha amesema, Chama cha CCM kinajihakikishia ushindi katika chaguzi zijazo, huku akibainisha kuwa kupata ushindi ni lazima isipokuwa ni ushindi wa asilimia ngapi.
“Chama cha CCM tunajihakikishia ushindi kwetu ni lazima hatuna wasiwasi na hilo, isipokuwa tunachoangalia ni ushindi wa asilimia ngapi! Hivyo niendelee kuwaomba watanzania wote kwa ujumla kuendelea kukiamini chama hiki kwani kipo kwa ajili ya maendeleo ya watanzania wote na si kwa maslahi ya mmoja mmoja”, amesema Makalla.
Kati ya miradi ambayo CPA Makalla ameitembelea leo ni pamoja na kituo cha Afya cha Kinyerezi, kuangalia huduma zinazitolewa na kituo hicho, huku akiwataka watoa huduma kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa, kwani haitakuwa na maana kuwa na majengo na vifaa vizuri bila ya kutumia lugha nzuri.
“Niwaombe sana ndugu zangu watoa huduma katika Hospitali hii, kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma, kwani haitakuwa na maana kuwa na majengo na vifaa vizuri huku lugha inayotumiwa ikiwa si nzuri kwa wagonjwa”, ameongeza Makalla
Kati ya mradi mwingine aliotembelea ni pamoja na jengo la shule lililo katika mtindo wa ghorofa katika Shule ya Sekondari Minazi mirefu, lenye madarasa 20 na matundu ya vyoo 45, ambalo hadi sasa limefikia asilimia 90 ya ukamilikaji wake na kutarajiwa kumalizika Julai 30, 2024.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best