September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CPA Makalla amtaka Waziri Aweso kumaliza tatizo la maji Longido

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline. Arusha

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuongeza Kasi ya kushughulikia tatizo la maji katika eneo la Namanga Wilaya ya Longido, ili wananchi waondokane na changamoto hiyo.

Agizo hilo limekuja baada ya Mbunge wa Longido ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, kuelezea kuwepo na changamoto mbalimbali katika Jimbo hilo ikiwemo ya maji hali inayopelekea wananchi katika Jimbo hilo kupata shida ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Akitatua changamoto hiyo CPA Makalla, akiwa kwenye mkutano wa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla, akiwa kwenye mkutano na Mabalozi wa CCM na Wakuu wa Taasisi za kiserikali uliofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Longido leo Septemba 5, 2024.

CPA Makalla, alimpigia simu Waziri Aweso ili kuwapatia majibu ya changamoto hiyo wananchi, ambapo Waziri Aweso alikiri uwepo wa changamoto hiyo, huku akieleza kuwa, tayari suala hilo linafanyiwa kazi kwani tayari mkandarasi ameshapatikana hivi karibuni ataanza kazi katika mradi huo wa maji.

Aidha, CPA Makalla amesema ni vyema watendaji wakaendelea kufanya kazi zao kwa ufanisi ili kuweza kukiletea ushindi Chama hicho katika chaguzi za Serikali za Mitaa, huku alielezea dhamira ya CCM ni kuwa na idadi kubwa ya wana-Chama zaidi ya Mil 12 kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Amesema ni vyema wana-CCM wakaendelea kuhamasisha wengine kuweza kujiunga na Chama hicho, huku akieleza kuwa zipo sababu za kukisemea chama kwa Yale mazuri yanayofanywa na Serikali yake ikiwemo uendelezwaji wa miradi ya maendeleo inchini.

“Hadi tunapoelekea kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, CCM tunatarajia kuwa na wanachama zaidi ya Mil 12 na sababu za kuwa na wana-Chama hao zipo wazi kwani wanaona maendeleo yanayofanywa na CCM nchini hivyo niwaombe tuendelee kuhamasishana”, amesema CPA Makalla.

Pia amesema kuwa, kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Mabalozi wa CCM nchini, imeendelea kukiweka chama hicho madarakani kwa kuendelea kukisemea yale mazuri yanayofanywa na Serikali, huku akisema kuwa CCM ndiyo chama namba 9 duniani huku kwa upande wa Afrika kikiwa namba moja.