Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
TUME ya Taifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu(COSTECH)imesema mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, serikali imetenga shilingi bilioni 6.3 kwa ajili ya miradi ya utafiti wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Huku shilingi milioni 600 zikielekezwa katika miradi minne ya usalama wa chakula,ikihusisha udhibiti wa magonjwa ya mazao,uboreshaji wa uhifadhi wa chakula na ubunifu wa vyakula vyenye virutubishi vya hali ya juu.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 17,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt.Amos Nungu,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Tume hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha amesema kuwa kwa kuwekeza shilingi bilioni 2.3 kupitia Samia Commercialization Fund,serikali imewapa wabunifu wa Kitanzania fursa ya kuingiza bunifu zao sokoni, hii inasaidia kuondoa changamoto ya kukosekana na dhamana ili kupata mitaji.
Vilevile Dkt.Nungu amesema kuwa COSTECH imeanzisha na kuziwezesha kongano nane bunifu katika mikoa ya Kigoma, Geita, Mafia, Mbeya, Dodoma, Morogoro, Singida na Pemba ili kusaidia sekta ya viwanda na kilimo. Miradi hii imewezeshwa kwa ufadhili wa shilingi milioni 750, kuhakikisha teknolojia bora zinatumika katika kuboresha uzalishaji wa mafuta ya mawese, dhahabu na mazao ya baharini.
“Kwa usimamizi thabiti wa serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,COSTECH imefanikiwa kuandaa mifumo ya usimamizi wa tafiti kwa kutumia teknolojia za kidijitali kupitia mradi wa HEET, pamoja na kuanzisha vigoda vya utafiti katika vyuo vikuu kama SUA na NM-AIST kwa ufadhili wa shilingi bilioni 4.7.
Pia amesema Serikali ya awamu sita imetoa fedha na kuweka mazingira rafiki kwa wanasayansi na wabunifu wa Kitanzania. Kupitia mfumo wa ushirikiano wa kimkakati kati ya serikali ya Tanzania na nchi rafiki pamoja na taasisi za kimataifa, COSTECH imepokea shilingi bilioni 5.65 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya utafiti wa pamoja kati ya watafiti wa Tanzania na washirika wetu.
Pamoja na hayo Dkt.Nungu amesema Serikali Katika kuimarisha miundominu ya utafiti, pamoja na kutoa fedha kwa vyuo vikuu imetoa bilion 9 kuhakikisha kuwa jengo la COSTECH linafanyiwa ukarabati na kujenga jengo jipya Dodoma.


More Stories
PAC yapongeza ujenzi nyumba 109 kwa waathirika wa maporomoko Hanang’
Rais Samia ataka watakao kwamisha huduma za ardhi kuchukuliwa hatua
Kapinga : Ni maono ya Dkt.Samia wananchi wote wapate umeme