Na Grace Gurisha, TimesMajira Online
TUME ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imewataka watafiti kujitokeza na kuandika maandiko ambayo yatawawezesha kupata takribani Sh bilioni 20 kwa ajili ya utafiti kwenye maneno yanayogusa jamii.
Hayo yamesemwa Juni 27/2022 na Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dkt. Amos Nungu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu fedha hizo zinazotolewa na Mabaraza ya Utafiti Duniani.
Amesema Costech ni miongoni mwa mabaraza ya utafiti 11 duniani ambayo wameweka fedha pamoja (Euro milioni nane) kwa ajili ya utafiti chini ya mwavuli wa ‘Global Research Counsel’ ambao ni mwavuli wa mabaraza yote ya utafiti duniani.
Dkt. Amesema kati ya nchi hizo, afrika ipo Tanzania, Kenya na Côte d’Ivoire, pia kuna nchi kutoka mabara ya Ulaya, Asia na Amerika Kusini, nchi zingine ni Chile, China, Afrika Kusini, Switzerland, Sweden, Tanzania, Uturuki, Côte d’Ivoire , Kenya, Netherland na Norway.
Amesema nchi hizo zimeweka fedha pamoja kwa makubaliano kwamba kila nchi inafadhili watafiti kutoka nchini kwake, kwa kuunda timu ya pamoja ambayo iwe na nchi tatu, ambapo moja lazima itoke Kusini nyingine Kaskazini.
Dkt Nungu amesema ili kupata fedha hizo inawabidi watafiti mbalimbali nchini kujitokeza na kuandika maandiko ambayo yatashindanishwa na mengine katika maeneo yaliyotajwa yakiwemo ya ustawi wa binadamu, mazingira na uchumi endelevu.
Amesema mengine ni kwenye mifumo ya chakula, mifumo lishe, nishati na maendeleo ya mijini. Amesema fursa hiyo imefunguliwa toka Mei 15, 2022 inaenda hadi Agosti 28,2022 dirisha linafungwa kwa kuandika andiko la awali.
Amesema baada ya hapo mchakato unaofuata ni kuandika andiko rasmi na kwamba kwa atakayeshinda fedha hizo zitafadhiliwa mwakani mwezi Mei.
“Kikubwa kinachotakiwa katika kuomba ufadhili huu ni umahiri wa kuandika mradi, watafiti watakaofanikiwa nafasi hiyo Costech itaongea na serikali kuongeza fedha kwa sababu kwa watakaoshinda tume imetenga sh million 120 kwa mradi mmoja,”
More Stories
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji
Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika
Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba