Na Jackline Martin, TimesMajira OnlineĀ
Tafiti zinaonyesha 80% ya uchafuzi wa bahari unasababishwa na shughuli za nchi kavu hivyo watanzania wametakiwa kuendelea kutunza mazingira ya bahari kwa kuhifadhi uchafu unaotumika katika vyombo vya melini na majumbani kwa kuweka miongozo na usimamizi iliyo bora ili kutoathiri mazingira ya bahari.
Hayo ameyasema leo Julai 25, 2022, Kaimu Mkuu wa chuo cha Bahari Dar es Salaam, Dkt. Tumaini Gurumo, wakati wakiadhimisha siku ya Bahari Afrika yenye Kaulimbiu inayosema ‘Kuhuisha mpango wa pamoja kwaajili ya kuitumia bahari’ na kuongeza kuwa ili kuendeleza uchumi wa Buluu nchi za Afrika zinapaswa kuangalia namna nzuri ya kutumia bahari kwa kuzingatia mabadiliko ya kimazingira kwani fursa nyingi za maendeleo ziko baharini.
“Tafiti zinaonyesha 80% ya uchafuzi wa bahari unasababishwa na shughuli za nchi kavu hivyo Kunahaja shuhuli zote zinazofanyika nchi kavu ziekewe miongozo na usimamizi ili kupunguza makali ya kemikali zinazoingia baharini”Alisema Dkt. Gurumo na kuongeza kuwa;
“Ni jukumu letu moja kwa moja kwasababu mimi inawezekana siyo mchafunzi wa moja kwa moja wa mazingira lakini naona wengine wakichafua, ninaponyamaza maana yake nitakua sijasaidia katika suala hili la utunzaji mazingira, wapo wanaokata mikoko, wanaotupa plastiki baharini, wanaomwaga mafuta, lakini pia wanaoharibu mazalia ya samani kwa kufanya uvuvi usiokubalika”
Aidha Dkt. Gurumo amesema katika kuhakikisha mazingira ya bahari yanatunzwa, Chuo cha Bahari kimekua kikifanya jitihada kubwa katika kutoa elimu na mafunzo katika upande wa bahari ikiwemo masuala ya utunzaji wa mazingira hayo;
“Kwa sasa tupo katika hatua za kuanzisha kozi ambazo zitakua zinazungumzia namna bora ya utunzaji wa mazingira ambapo zitawafaa sana watu mbalimbali katika maeneo yetu ya Tanzania kwa maana ya kwamba tunao upungufu mkubwa wa wajuzi wenye weledi katika eneo la masuala ya utunzaji wa mazingira ya Bahari”
Pia Dkt. Gurumo amesema katika chuo hicho wanayo Club ya mazingira ambayo ipo njiani kuanzishwa yenye lengo la kushirikisha wanafunzi wao pamoja na walimu.
“Tunataka tuipeleke elimu hii ya utunzaji wa mazingira kuanzia watoto wadogo kwenye shule za awali waweze kutambua Habari ya mazingira”
Kwa upande wake Mhadhiri Msaidizi katika chuo cha Bahari Dar es Salaam, Mhandisi Daniel Rukonu amesema wanatoa kozi ambazo zinasaidia hasa jamii ya watanzania kupata wazawa ambao wanaubobezi katika fani za uhandisi wa meli, usafirishaji wa mizigo ya bahari na katika fursa za kutunza mazingira pamoja na kuchimba rasilimali za mafuta na gesi;
“Chuo chetu kinafundisha kozi za usalama baharini na kutunza mazingira ambapo kama chuo tunawaomba wananchi na watanzania kwa ujumla waweze kutunza mazingira ya bahari na kuweza kutunza uchafu ambao unatumika katika vyombo vyote vya melini na majumbani”
Aidha Rukonu Amezitaja faida na fursa ambazo zinapatikana katika uchumi wa Buluu;
“Kama nchi tunapata chakula kutoka bahari ambao ni samaki,fedha za kigeni kupitia utalii, tutafaidika na uchumi wa Buluu kupitia mizigo ambayo tunaisafirisha kutoka ng’ambo mashariki ya mbali kuja kwetu kupitia fedha za kigeni ambazo tunazipata kupitia bandari yetu ya Dar es salaam lakini pia kodi tunayopata kupitia mizigo na usafirishaji”
Kila Julai 25 nchi za Afrika huadhimisha siku ya bahari ambao ni mpango wa maendeleo endelevu ya kukuza uchumi kupitia mpango wa miaka 50.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja