Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Chunya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya imefunga kitabu cha Mahesabu ya mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwa inadaiwa zaidi ya sh. Bilioni 2 na wadau mbalimbali wakiwemo wazabuni, mishahara na stahiki za watumishi.
Hayo yamejiri kwenye kikao maalum cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chunya mkoani Mbeya cha kujadili na kupitisha hesabu za mwisho wa mwaka wa fedha 2023/2024.
Akitoa taarifa za kufunga hesabu kwa madiwani wa halmashauri hiyo Mhasibu wa halmashauri Rajab Lingoni amesema katika mwaka wa fedha ulioisha 2023/2024 halmashauri ilikusanya jumla ya sh. Bilioni 7.1.
Lingoni amesema hadi kufikia Juni 30, 2024 halmashauri ilikuwa inadaiwa Zaidi ya sh. Bilioni 2.1, fedha zilizotokana na madai mbalimbali yakiwemo malimbikizo ya mishahara ya watumishi wake na wazabuni.
“Mheshimiwa mwenyekiti kati ya fedha hizo madeni ya malimbikizo ya mishahara ni sh. Milioni 260, madeni ya wazabuni na watoa huduma mbalimbali ni sh. Milioni 145, madeni ya stahiki za watumishi ikiwemo uhamisho, Mafunzo na matibabu ni sh. Milioni 716, pia deni la mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ni sh. Milioni 630,”amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chunya,Mbarak Alhaji Batenga pamoja na kuipongeza halmashauri hiyo kwa makusanyo mazuri, ameiagiza kulipa fedha hizo ili kuwapa motisha ya kufanya kazi watumishi na kuongeza ufanisi kwenye halmashauri hiyo.
Aidha kiongozi huyo wa wilaya ameiagiza halmashauri hiyo kuanza kufikiria kuboresha miundombinu ya elimu ili kuwa tayari kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza, darasa la awali na kwanza kwa mwaka wa masomo 2025.
“Sipendi tuanze kufuta likizo za watu ili wakimbizane kujenga vyoo au vyumba vya madarasa, ningependa halmashauri tuanze kujiandaa saizi ili muda ukifika wa kuwapokea wanafunzi tusianze kukimbizana na kufuta likizo za mwisho wa mwaka kwa hiyo kwa hili ninawasisitiza sana’’ amesema.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chunya Bosco Mwanginde amesema wapokea maelekezo yote na wapo tayari kuyafanyia kazi.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best