Na Mwandishi wetu, timesmajira
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo amesema Watanzania kwa ujumla wameonesha utayari na uhitaji mkubwa wa kuona uwekezaji na uendeshaji utakaoleta maboresho, ufanisi na kuongeza mapato katika Bandari ya Dar es Salaam.
Pia ameielekeza Serikali kuharakisha utekelezaji wa hatua mbalimbali zilizobakia za uwekezaji bandarini ili wananchi waanze kuona matokeo.
Chongolo ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano mkubwa uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati akihitimisha ziara yake iliyotumika kuwapatia elimu wananchi kuhusu makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai, yanayolenga kuweka msingi wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuboresha utendaji na ufanisi wa kazi bandarini hapo.
“Msimamo wa Chama Cha Mapinduzi kuhusu uwekezaji wa bandari ni kuitaka serikali kuhakikisha kasi ya utekelezaji wake iende kwa haraka iongezwe ili tuanze kupata manufaa na matokeo kwa haraka. Tunasema hivyo kwa sababu msingi wake ni Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020/25 tuliyoinadi na kupitishwa na wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na kwetu kwenye suala la utekelezaji wa ilani mtu yeyote akitaka kutukwamisha ni lazima tusimame kuwa kitu kimoja tushikamane tuhakikishe haturuhusu fitina, hila, maneno ya uchokozi ili tusifanikishe hilo na kwenye hili wana CCM wameonesha kwa dhati kabisa kulikubali na kuwa kitu kimoja, niwashukuru sana,”amesema na kuongeza
“Wananchi na wanaCCM wameonesha utayari mkubwa sana, wameonesha uhitaji mkubwa wa kuona mabadiliko na tija tunayoizungumzia kwenye uwekezaji wa bandari ikitokea kwa haraka, niwapongeze sana kwenye maeneo yote tuliyopita. Chama Cha Mapinduzi tunasema hili ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020/25 kwa sababu kwenye ibara ya 22 na 59 tumeahidi na tulieleza kwa kina mpango wa suala hilo. Msimamo wa Chama Cha Mapinduzi kuhusu uwekezaji wa bandari ni kuitaka Serikali kuhakikisha kasi ya utekelezaji wake iende kwa haraka iongezwe ili tuanze kupata manufaa na matokeo kwa haraka,” amesema Chongolo.
AmesemayCCM inasisiitizia serikali kuweka msukumo katika hatua zinazoendelea ili kama kuna jambo au maoni ya kuongeza tija kwenye kuboresha mkataba yachukuliwe yawekwe ili kuwapeleka kwa spidi kule wanapotaka. “Sasa kuna watu wametoa maoni ya aina mbalimbali kuna watu wamesema uwekezaji huu ni muhimu sana lakini kwenye ule mkataba kuwe na mambo kidogo yanayoendana na kile wanachokipendekeza, hayo ndiyo mawazo ya msingj yenye tija,”amesema na kuongeza
“Na sisi CCM tunaiagiza serikali pia kuhakikisha inatekeleza hilo na kufanya mapitio kuangalia mazingira na kuona umuhimu wa kuyaruhusu mawazo yenye tija kuingia na kuchangia uboreshaji wa mkataba huu ili utufikishe kule ambapo tutapata tija na matokeo makubwa zaidi. Tunasema hivyo kwa sababu mkataba sio Msahafu wala Biblia, hatuwezi kushikilia tukasema aah hauna dosari…hapana, umeandikwa na wanadamu, macho na elimu vinatofautiana na elimu inatofautisha watu kuona mambo kwa namna tofauti,” amesema Katibu Mkuu wa CCM,”amesema Chongolo.
Mbali ya kuielekeza Serikali kuzingatia na kufanyia kazi maoni chanya na yenye tija yanayotolewa kuboresha uwekezaji, Katibu Mkuu, Chongolo alisema uwepo kwa kundi dogo la wanasiasa na wanaharakati wanaopita na kutumia majukwaa mbalimbali kufanya upotoshaji na kufanya uchonganishi, wakilenga kupinga suala hilo muhimu lenye maslahi makubwa kwa taifa lisifanyike na baada ya hoja zao zote kujibiwa, sasa kundi hilo limeanza kutumia lugha za matusi dhidi ya viongozi wakuu wa nchi, waliopo madarakani, waliostaafu na wale waliotangulia mbele ya haki.
“Kuna kundi la pili ambalo lenyewe linapinga tuu…mwanzo lilianza kwa kukosoa mkataba. Baada ya kuona kwenye mkataba wanakosa eneo la msingi la kusimamia sasa wamebadilika wanaenda wanasema hakuna uwekezaji huu kufanyika, eti hauna tija. Maana yake ni nini…maana yake CCM tusitekeleze ilani yetu kwa kiwango cha juu chenye tija ili wakija wawe na kazi rahisi ya kuichonganisha CCM na wananchi wasitupatie ridhaa kwa mara nyingine. Sasa nani yupo tayari kuchonganishwa? Hatupo tayari. Tuliahidi na tutatekeleza kwa hiyo serikali lazima itekeleze kwa kishindo,”amesema na kuongeza
“Sasa hawa jamaa wamegundua msimamo wetu umenyooka na hatuyumbi wameamua sasa kuanza matusi na wanatukana kweli, hadi mara nyingine unajiuliza huko duniani kuna chuo kinachotoa shahada ya matusi? Kwa sababu ukiangalia namna wanavyopanga na kuyasema vizuri hayo matusi unajiuliza hawa wenzetu hii professional (taaluma ya kutukana) wameisomea wapi,” amesema Chongolo,
Amesema kuwepo kwa kundi la watu wanaopinga kila jambo kubwa, lenye malengo mazuri ya kuimarisha misingi ya kujenga mazingira ya fursa za maendeleo ya watu na ustawi wa Tanzania, haijaanza kwa mradi wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, akitolea mifano ya jinsi baadhi ya wanaharakati na wanasiasa wa vyama vya upinzani kwa kushirikiana na watu kutoka nje ya Tanzania walivyowahi kupinga miradi mingine ya uwekezaji mkubwa wenye manufaa ya nchi, ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere na Reli ya Kisasa (SGR) na Bomba la Mafuta la Uganda – Tanzania.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa