December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CHONGOLO:CCM itaendelea kulinda na kudumisha uhuru wa nchi na raia wake

Na Penina Malundo,Timesmajira, Online

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Daniel Chongolo amesema katika kuadhimisha miaka 45 ya Chama cha CCM, Chama hicho kinajivunia kulinda na kudumisha uhuru wa nchi, raia wake na kuendelea kusimamia Muungano wa Tanzania ikiwa ni moja ya tunu za Watanzania katika kusimamia ujenzi wa taifa na kuwaunganisha kwa tamaduni zao.

Pia amesema Chama hicho kinatarajia kufanya zoezi la uzinduzi wa kadi za kieletroniki Februari 5 mwaka huu mkoani Mara ambapo wakereketwa na wananchi katika mikoa 32,wameweza kumuunga mkono Rais na Mwenyekiti wa Chama hicho, Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuchangia fedha kugharamia kadi hizo.

Akizungumza hayo jana,wakati akitoa hotuba katika uzinduzi wa Sherehe za uzinduzi wa Chama hicho katika kiwanja cha Mwehe Makunduchi wilaya ya Kusini Unguja Mkoa wa Kusini.

“leo ni siku muhimu sana kwa wanaCCM wote nchi nzima, Tanzania bara na Zanzibar kwani ndio tunazindua rasmi maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi ambacho ni zao la vyama vyetu vya ukombozi, Afro Shiraz Party (ASP) na Tanganyika African National Union (TANU) na kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tarehe 5 Februari 1977 hapa Zanzibar katika Uwanja wa Amani,”alisema na kuongeza

“WanaCCM tunayo kila sababu ya kuadhimisha na kusherehekea siku hii adhimu ya kuzaliwa kwa chama chetu kila ifikapo Februari,5 ya kila mwaka ambapo unapata nafasi ya kupima na kutathimini pale tulipotoka na tulipo,”alisema

Chongolo amesema miaka 45 ya CCM nchi inajivunia kujitawala na kuongozwa kwa misingi ya kijamaa na kidemokrasia huku tukiendelea mapambano dhidi ya maadui watatu umaskini, ujinga na maradhi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi.

“Chama chetu kimeendelea kuongoza jamii inayozingatia usawa kwa raia wote, bila kujali jinsi, rangi, kabila, dini au hali ya mtu na kusimamia ukomeshaji wa vitendo vyote vya dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu na upendeleo miongoni mwa jamii katika kipindi chote kilichopo nchini,”amesema na kuongeza

” Vyama viwili vya ukombozi vya ASP na TANU, vinaungana idadi ya wanachama ilikuwa ni ndogo, lakini sasa CCM inao wanachama takribani milioni milioni 15, wenye kadi na wanaolipa ada za uanachama, hao ni mbali na wakereketwa na wapenzi wa chama,”amesema

Akizungumzia Mafanikio,Chongolo amesema wanaCCM wote nchi nzima wanajivunia mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na chama chao,ikiwa ni pamoja na kuaminiwa na umma wa Watanzania na kupewa dhamana kupitia sanduku la kura, hivyo kukabidhiwa ridhaa ya kuunda serikali, kushika na kuongoza dola.

“CCM kimeendelea kusimamia kuwepo kwa mazingira na fursa za Watanzania kujipatia maendeleo katika nyanja zote zikiwemo, afya, elimu, miundombinu ya barabara, mawasiliano, kilimo, nishati, usafiri wa reli na anga, ukuaji wa masoko kwa mazao ya biashara, uvuvi, ukuaji na ustawi wa diplomasia ya kiuchumi na ushirikiano wa kimataifa,”amesema

Amesema Mwaka 1981 chama kilifanya mageuzi na kujitathmini kifikra na kutoa mwongozo wa CCM wa mwaka 1981 ambao kwa ujumla ulibeba fikra za kujikosoa na kukosoana kuwa ni silaha ya uanamapinduzi.

Akizungumzia madhumuni ya maadhimisho hayo ya kuzaliwa kwa CCM mwaka huu, ni kutoa uelekeo katika masuala ya msingi ya chama katika kusimamia kwa ufanisi zaidi malengo makuu ya mradi wa awamu ya nne ya kujenga na kuimarisha chama, hasa kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu ndani ya Chama.

Pia amesema madhumuni mengine ni kuongeza idadi ya wanachama na kuwahamasisha kulipa ada kwa wakati na kuifanya shughuli ya usajili wa wanachama wa CCM na jumuiya zake kwa kutumia mfumo wa TEHAMA na utoaji wa kadi za kielektroniki kuwa ni endelevu na kudumu.