November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo: Viongozi wa CCM simamieni mali za Chama kiuadilifu

Na Penina Malundo, Timesmajira,Online

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewaonya wote wenye dhamana ya kusimamia mali za Chama wafanye kwa uadilifu kwani hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kupoteza nyaraka za mali hizo.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam leo wakati akiweka jiwe la msingi ya ujenzi wa ofisi CCM wilaya na nyumba ya Katibu Mkuu wa Chama mkoa wa Dar es Salaam zilizopo wilayani Kigamboni.

Amesema  mwaka 2017-2018, Chama kilifanya kazi ya kutambua  mali na rasilimali zake na kutengeneza orodha ndefu na kuwekwa mpango wa kuzisajili  ambao ulikamilika.Chongolo amesema baada ya usajili kukamilika Chama kiliamua kutengeneza utaratibu wa kuzimiliki mali hizo kisheria.

“Jambo linalosikitisha ni kasi katika maeneo mbalimbali  ya kuendelea kutafuta nyaraka za umiliki kisheria  wa maeneo imepungua na baadhi wameanza kuacha na  kuona sio sehemu ya majukumu yao,” amesisiitiza.

Aidha amesema moja ya kigezo watakachompima mtendaji wa Chama katika ngazi yotote ni namna anavyoshiriki katika kila eneo ambalo limeandikwa kuwa sehemu ya wajibu wake na siyo vinginevyo.

“Inasikitisha kuona mali tulizomiliki kwa karne, kwa miaka mingi, leo mtu anajitokeza  na kusema hapa kwangu na sio ajabu kwa kutamka hivyo anapata fursa  ya kusumbua na hata kutengeneza mazingira  na kujitengenezea  uhalali, wakati wenye mali ambao ni Chama ngazi husika wapo na wanayaona hayo wamekaa kimya na wanasubiri miujiza, hili hatutalikubali,” amesema.

Chongolo amewahakikishia wana CCM kuwa litakapotokea tukio la namna hiyo hatua kali zitachukuliwa kwa mtendaji aliyepo katika ngazi husika na kwenye hilo hatakuwa na mzaha.

Akizungumzia Chaguzi ndani ya CCM amesema Chama hicho bado kinakabiliwa na changamoto ya rushwa katika ngazi ya wilaya kwani  walibaini baadhi ya watu kufanya rafu za kikiuka taratibu za uchaguzi na kufuta matokeo ya wilaya 21 na uchaguzi kurudiwa.

“CCM ina bahati ya kuwa na wanachama wengi, wazuri, wenye uwezo  mzuri  wa kiakili, kiuongozi na wenye moyo na mapenzi mema na dhati kwa Chama,”amesema