December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo afanya mazungumzo na mabalozi wa nchi tano

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa nchi tano za Kusini mwa Bara la Afrika kutoka mataifa ya Angola, Namibia, Afrika ya Kusini, Msumbiji na Zimbawe, ambapo pamoja na masuala mengine yamelenga kufanya tathmini, kuendeleza ushirikiano na kuboresha uendeshaji wa Chuo ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere (MJNSL), iliyopo Kibaha, mkoani Pwani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM Lumumba, jijini Dar es Salaam, Chongolo amekutana na Balozi Luteni Jenerali (Mstaafu) Anselem Sanyatwe – Zimbabwe,Balozi Lebbius Tangeni Tobias – Namibia, Balozi Sandro Renato Agostinho De Oliveira – Angola, Balozi Ricardo Mtumbuida – Mozambique na Kaimu Balozi Stella Vuyelwa Dhlomo-Imieka wa Afrika ya Kusini.
Chuo hicho cha MNJSL kilichoko Kwa Mfipa – Kibaha, Mkoa wa Pwani, nchini Tanzania, kinaendeshwa kwa ushirikino wa Vyama Sita vya Ukombozi Kusini mwa Afrika, ambavyo ni CCM -Tanzania, ANC – Afrika ya Kusini, FRELIMO – Msumbiji, SWAPO – Namibia, ZANU – PF – Zimbabwe, MPLA – Angola.
Akizungumza kwa niaba ya mabalozi hao, Balozi wa Msumbiji nchini, Ricardo Mtumbuida amesema kuwa vyama hivyo sita vya ukombozi ambavyo vinashirikiana kuendesha Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, vinajukumu mahsusi la kuwaongoza vijana wa sasa kuendelea kuwa wazalendo, wenye mapenzi mema na kujali maslahi ya Bara la Afrika.
Aidha, Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Ngemela Lubinga akizungumzia kikao hicho na kujibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu miaka 30 ya demokrasia ya vyama vingi nchini, amesisitiza kuwa CCM na vyama vingine vya ukombozi vina jukumu la kuendelea kuwatumikia na kuwaongoza wananchi kwa haki na kidemokrasia wakati wote ili kuweka mazingira ya ustawi na maendeleo yanayotarajiwa.