Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mary Chatanda amesema ameridhishwa namna watu walivyojitokeza kwenye zoezi la upigaji kura wa kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 27, 2024 mara baada ya kupiga kura kwenye Kituo cha Majengo mjini Korogwe, Chatanda alisema wananchi wanatakiwa wajue haki ya kupiga kura kwa viongozi wanaowataka ili kuwasaidia kusukuma maendeleo, ni jukumu la kwao wananchi.
Chatanda ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), na Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema wananchi wanatakiwa kujenga utamaduni wa kupenda kuchagua viongozi kwa njia za demokrasia sababu maendeleo yanatokana na ushirikiano kati ya viongozi na wananchi wa mtaa husika.
“Suala la kumchagua kiongozi wa mtaa ni jambo muhimu sana kwa maendeleo yako ya mtaa wako. Unapomchagua Mwenyekiti wa Mtaa maana yake wewe umechagua maendeleo. Maendeleo yeyote yanatokana na uongozi uliopo kwenye mtaa pamoja na wananchi. Mnapokaa kwa ajili ya kupanga mambo yenu ya maendeleo, mnapanga kuanzia kwenye mtaa, inakwenda kwenye kata, na ndipo mnakwenda halmashauri.
“Kwa hiyo ni jambo muhimu sana kwa wananchi kujitokeza kuja kupiga kura. Lakini hali inavyoonesha hapa muonekano ni nzuri, na watu wamejitokeza kuja kupiga kura. Wito wangu kwa wananchi waweze kujitokeza kwa uchaguzi huu na chaguzi nyingine, na viongozi wa vyama vya siasa wamehamasisha sana kilichobaki ni wananchi wajitokeze kwa wingi kuja kuchagua viongozi wanaowapenda” alisema Chatanda.
Naye Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Mji Korogwe Mwashabani Mrope akizungumza na mwandishi wa habari hii mara baada ya kutembelea baadhi ya vituo, alisema muitikio wa wananchi ni mkubwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka huu, kwani baadhi ya vituo kwenye mitaa na kata wananchi wamejitokeza kwa wingi.
“Nimepita kwenye mitaa ya kata za Masuguru, Majengo na Kilole nimeona muitikio ni mkubwa, na wananchi wameonesha wana dhamira ya dhati ya kuwachagua viongozi wao wa mtaa.
“Timu yetu ya Halmashauri ya Mji Korogwe tulihakikisha tunatoa matangazo kwa njia mbalimbali ikiwemo michezo na mabonanza ili kuwahamasisha wananchi, kwanza kujiandikisha halafu kupiga kura. Lakini pia tulitangaza kwa kutumia magari, na mabango kuweka kwenye mitaa mbalimbali, na mafanikio yake tumeyaona” alisema Mrope.
Naye mgombea nafasi ya Mwenyekiti Mtaa wa Majengo kwa tiketi ya CCM Hadija Mbwana amesema ameridhika na utaratibu wa upigaji kura, kwani wananchi wanafika kwenye kituo na kuangalia majina yao yaliyobandikwa kwenye mbao za matangazo, na akishapata namba yake anaingia kupiga kura.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango