Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa katika kuhakikisha wananchi wa Jiji la Mwanza wanapata maji ya uhakika, mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji Butimba ni sehemu ya maboresho ya hupatikanaji wa huduma za maji katika mji wa Mwanza.
Kukamilika kwake itasaidia kupunguza makali ya mgao na kukosekana kwa maji katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Mwanza ambapo mahitaji ya maji kwa siku ni lita milioni 154 huku kwa sasa chanzo kilichopo cha Capripoint kinauwezo wa kuzalisha lita millioni 90 kwa siku.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Mwakilagi na Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo ya kutembelea mradi huo na kujionea maendeleo ya utekelezaji wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele, amesema
utekelezaji wa mradi huo ulianza Februari 2021 na natarajiwa ukamilike mwishoni mwa Januari 2023.
Mhandisi Msenyele, amesema kutokana na uzalishaji mdogo ndio sababu ya kuwepo kwa mgao mkali wa maji katika Jiji la Mwanza,lakini mradi huo utaleta matumaini makubwa na utapunguza makali,zaidi wakifanya upanuzi kwenye hicho chanzo watahakikisha wanazalisha maji yanayotosheleza wananchi wa Jiji la Mwanza na mengine ya ziada.
Amesema mradi huo ambao unagharimu kiasi cha bilioni 69,ambapo wanajenga chanzo cha kutibu maji kwa kuanzia kuchukua maji kutoka kwenye ziwa,kuja sehemu ya mitambo ya kutibu maji pia kutakuwa na sehemu ya kuhifadhia maji yaliyotibiwa kwa maana ya tenki la kuhifadhia maji.
Pia amesema,chanzo hicho kinajengwa kwa mfumo wa kusanifu na kujenga,kwa maana mkandarasi ndio mwenye kusanifu mradi vile vile na kujenga miundombinu, ambapo kukamilika kwake kutaongeza uzalishaji wa maji kutoka chanzo cha maji Capripoint cha sasa kinachozalisha lita za maji milioni 90 kwa siku hadi kufikia lita za maji milioni 138.
“Uwezo wa chanzo cha Butimba awamu ya kwanza itakuwa lita za maji milioni 48,kwaio tutakuwa na uwezo wa kuzalisha lita za maji milioni 138 kwa siku huku mahitaji ya maji kwa Jiji la Mwanza ni lita za maji milioni 154 kwa siku,pamoja na kukamilika kwa chanzo hiki kutakuwa na upungufu wa lita za maji milioni 16, lakini si haba mpango kazi wa hiki chanzo ni kwamba tujenge kwa awamu,baadae upanuzi wake wa kuongeza lita milioni 160, ambao ni uwezo wake mkubwa ili kuongeza hali ya upatikanaji maji kwa Jiji la Mwanza,”amesema Mhandisi Msenyele.
Hata hivyo amesema,utekelezaji wa mradi huo unatokana na fedha za mkopo nafuu unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania ikishirikiana na wafadhili wa maendeleo kwa maana ya Benki ya Uwekezaji ya Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa,unatekelezwa na kampuni za kutoka Ufaransa ambazo ni Sogea Satom na Vinci Construction huku kazi nyingine wamekuwa wakiwapa wakandarasi wazawa.
Mhandisi wa Mkandarasi wa kampuni ya Sogea Satom,Cyrus Maina,amesema katika mradi huo upande wa usanifu umefikia asilimia 80 huku ujenzi ndio umeanza ambao umefikia asilimia 10 na wanatarajia kukamilisha kwa muda na wakandarasi wanaendelea kujitahidi ili mradi huo usichelewe na watu wa Mwanza waweze kupata maji.
“Kwa upande wa ujenzi tutaweka bomba la kilomita moja ndani ya ziwa,ili kuweza kuchukua maji safi ndani ya ziwa na kupunguza gharama za kuyasafisha maana ukiyachukua ndani hayatakuwa na uchafu mwingi,baadae tutakuwa na bomba ambalo litatoa maji hapo mpaka kwenye chanzo ambayo yanasafishwa kisha kupelekwa katika sehemu tutakapo ya hifadhi kwa muda mfupi kabla ya kupitishwa kwenye maboba hadi kwenye matenki mawili ya Igoma na Nyegezi,”amesema Maina.
Akizungumza baada ya kutembelea na kujionea namna utekelezaji wa mradi huo unavyoendelea Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Mwakilagi, amesema wameridhika na namna utekelezaji wa mradi huo unavyofanyika.
Suala la kupeleka huduma kwa wananchi ni jambo ambalo lipo katika ilani ya CCM ambayo inaeleza kufikia 2025 suala la changamoto ya maji inakuwa historia katika maeneo mbalimbali hivyo utekelezaji wa mradi huo ni ahadi ya CCM na Rais ameisha utangazia umma suala la kumtua mama ndoo kichwani ni ajenda yake.
Mbali na mradi huo wa chanzo cha maji pia walitembelea mradi wa kulaza bomba na booster station( kituo cha kusukuma maji) ambao umefikia asilimia 98, ambapo bomba hilo linategemea maji kutoka kwenye chanzo cha maji Butimba.
Sababu ya miradi hiyo kushindwa kukamilika kwa pamoja ni kutokana na lakini changamoto iliojitokeza baada ya kutangaza zabuni,(tender) kwa mara ya kwanza kwa mradi wa chanzo cha maji Butimba walijitokeza wakandarasi wasiyo kuwa na sifa ikabidi waanze mchakato mpya ambao ulichukua takribani miezi 9.
More Stories
Kamati ya Mfuko wa Jimbo Musoma Vijijini yagawa vifaa vya ujenzi
Hatma mrithi wa Kinana kupatikana
Mrithi wa Kinana CCM kujulikana katika Mkutano Mkuu wa Jan 18/19