Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Changamoto ya upungufu wa dawa inaenda kuwa historia nchini baada ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi kupiga marufu utolewaji wa fomu namba 2C kuanzia July 1, 2022 ambayo ilikua ikitoa mwanya kwa baadhi watoa huduma kufanya udanganyifu.
Marufuku hiyo ameitoa kwenye kikao na watumishi wa Afya mkoani Kigoma kilichohudhuriwa pia na Mganga mkuu wa Mkoa Kigoma Dkt. Jeska Leba Baada ya kufanya ziara fupi katika hospitali hiyo.
Prof. Makubi amesema kuwa kuna baadhi ya watoa huduma wamekuwa wakitumia fomu hiyo vibaya kwa kuwaandikia dawa wagonjwa kwenda kununua nje ya kituo cha kutolea huduma ya Afya cha Serikali.
“Hii imekua ni uchochoro kwa wapigaji lakini pia ni usumbufu kwa mgonjwa kwenda kununua dawa nje, hivyo dawa zinatakiwa zijazwe kwenye hospitali za Serikali na kuacha kuwanufaisha wengine.” Amesema Prof. Makubi
Aidha, katika kikao hicho Prof. Makubi amebainisha mambo kadhaa muhimu ya kuzingatia kwa watumishi hao wa Afya ikiwemo kuhakikisha sekta ya Afya inafanya vizuri katika uongozi na uwajibikaji kwenye kutoa huduma nzuri.
Pia, kuwa na lugha nzuri wakati wa kutoa huduma, kuwajibika kazini, kuhakikisha ubora wa huduma za tiba na kinga, ukaguzi wa mara kwa mara, kuendelea kutoa chanjo pamoja na elimu za chanjo mbalimbali na kujali Afya ya mama na mtoto.
Prof. Makubi katika ziara hiyo ametembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi na ukarabati wa majengo na kubaini baadhi ya changamoto ikiwemo ya mradi wa Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) linalosuasua na kutoa maagizo hadi ifikapo Juni 30, 2022 liwe limekamilika.
“Muache mazoea kwenye kazi, mmepewa kazi na hela zote mmelipwa nataka mkamilishe mradi wa jengo hili kabla ya Juni 30, 2022 fanyeni kazi usiku na mchana na ikiwezekana ongezeni vibarua.” Alisisitiza Prof. Makubi
Hata hivyo, Prof. Makubi amewasifu viongozi na watendaji wanaosimamia mradi wa ujenzi wa jengo la dharula (EMD) ambapo ujenzi wa jengo hilo unaendelea vizuri na umegharimu jumla ya shilingi Bilioni 1.3.
“Miradi yote hii mjitahidi muimalize kwa wakati. Mfanye kazi usiku na mchana, ongezeni vibarua kazi ikamilike bila kuharibu ubora kwa kuwa wananchi wanataka huduma bora ya yenye mazingira rafiki kwao.” Amesema Prof. Makubi
Miongoni mwa miradi ya majengo katika hospitali hiyo ya Rufaa Mkoa wa Kigoma ni pamoja na jengo la upasuaji, jengo la kutakasishia vifaa vya kutolea huduma (CSSD), jengo la Monchwari, jengo la dharula (EMD), jengo la wagonjwa wa nje (OPD) pamoja na jengo la tiba mtandao ambalo limekamilika kwa asilimia 100.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â