December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Changamoto ya upotevu wa mazao ya uvuvi yaanza kupatiwa majibu

Na Edward Kondela,TimesMajira online,Lindi

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (Mb) ameupongeza Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa kuyafanyia kazi maono ya serikali ya kuhifadhi mazao ya uvuvi ambayo yamekuwa yakiharibika kutokana na kukosekana kwa nyenzo za kuyahifadhi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega akizungumza na wanakijiji cha Songosongo kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo cha kuzalisha barafu kilichojengwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa ufadhili wa Climateworks Foundation na kuipongeza WWF kwa kuyafanyia kazi maono ya serikali ya kuhifadhi mazao ya uvuvi ambayo yamekuwa yakiharibika kutokana na kukosekana kwa nyenzo za kuyahifadhi ikiwemo barafu. Picha zote na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo juzi akiwa katika Kijiji cha Songosongo kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo cha kuzalisha barafu kilichojengwa na WWF kwa ufadhili wa Climateworks Foundation chenye thamani ya Shilingi Milioni 424, kwa ajili ya kuhifadhia samaki wanaovuliwa na wanakijiji hao.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (kushoto) akimshuhudia Mkurugenzi Mkazi wa WWF Tanzania, Dkt. Amani Ngusaru na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya na Kijiji cha Songosongo katika utiaji saini wa makabidhiano ya kituo cha kuzalisha barafu kilichopo Kijiji cha Songosongo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo hicho.

Amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2021/22 imeweka mipango mbalimbali ya kuhakikisha inaongeza vituo vya kuhifadhia mazao ya uvuvi ili wavuvi waondokane na changamoto ya samaki kuharibika kutokana na ukosefu wa barafu na maeneo ya kuyahifadhia mazao hayo.

“Hali duni inachangiwa na upotevu wa mazao wanayovua kutokana na uvuvi na pia kutokuwa na uhakika wa masoko ya mazao wanayoyapata ndiyo maana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inakuja na suluhu kuokoa wavuvi na watanzania kwa ujumla wake,” amesema Ulega.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (kushoto) akipeana mkono na Mkurugenzi Mkazi wa WWF Tanzania, Dkt. Amani Ngusaru mara baada ya Dkt. Ngusaru kuzungumzia mradi wa miaka miwili wa WWF katika kijiji cha Songosongo kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, uliowezesha kupatikana Tani 91,000 za samaki aina ya pweza zenye thamani ya Shilingi Milioni 458, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo cha kuzalisha barafu kijijini hapo

Aidha,katika kuhakikisha mazao ya uvuvi yanakuwa na masoko ya uhakika Ulega alisema azma ya wizara hiyo ni kuona mazao hayo yanasimamiwa na ushirika hali ambayo itasaidia kuwa na umoja ambao utawezesha wavuvi kusikilizwa na kupata masoko kwa pamoja.

Pia amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itakuja na mkakati wa usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya vichanja maalum kwa ajili ya kukaushia dagaa na samaki ili kuzuia mazao hayo kutokuwa na mchanga na kuyaongezea thamani kwa kupata masoko zaidi ndani na nje ya nchi hali itakayobadilisha uchumi wa wavuvi na serikali kupata mapato zaidi.

Kuhusu zao la mwani ambalo wanakijiji cha Songosongo wamelalamikia kukosa masoko hali inayosababisha nyumba zao kurundikana zao hilo na hatimaye kuharibika na wakati mwingine kuuza kwa bei ndogo, Naibu Ulega alisema katika kipindi hiki wizara itapitia upya sheria inayosimamia zao la mwani ili kubaini changamoto ambazo ni kero kwa wafanyabiashara wa zao hilo na kuziondoa ili wakulima wa mwani na wafanyabiashara waweze kunufaika.

“Moja ya jambo ambalo pamoja na kutafuta soko la mwani tutengeneze kiwanda kidogo cha kukausha mwani na kuliongezea thamani zao hilo ili wakulima waweze kuhifadhi vizuri mwani na kuuza kwa bei nzuri zaidi kuelekea katika uchumi wa bluu.” amefafanua Ulega.

Ameongeza kuwa kupitia zao la mwani wanakijiji cha Songosongo wataweza kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na mwani ikiwemo sabuni na kuuomba Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kufikisha elimu ya ujasiriamali kwa wanakijiji hao juu ya masuala ya ujasiriamali.

Naibu Waziri Ulega pia amesema ni wakati muafaka kwa Serikali kuangalia upya Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) badala ya kulinda rasilimali za uvuvi pekee viweze kunufaika kwa kupata mikopo na kuendesha shughuli zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa WWF Tanzania Dkt.Amani Ngusaru amesema kituo cha kuzalisha barafu kilichojengwa katika Kijiji cha Songosongo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi chini ya ufadhili wa Climateworks Foundation chenye thamani ya Shilingi Milioni 424, kina uwezo wa kuzalisha barafu Tani 1.4 kwa saa 24.

Dkt.Ngusaru alisema mradi huo umeenda sambamba na uhamasishaji wa ufungaji wa miamba ya samaki aina ya pweza ambapo inakadiriwa kwa kipindi cha miaka mwili ya mradi, Tani 91,000 za pweza zimevuliwa katika Kijiji cha Songosongo zenye thamani ya Shilingi Milioni 458, ambapo fedha hizo zimetokana na ufungaji wa miamba kwa awamu tano.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei amesema ili kuhakikisha kituo cha uzalishaji barafu kilichopo katika Kijiji cha Songosongo kinakuwa na tija ni lazima uvuaji wa samaki aina ya pweza uwe endelevu na kuhakikisha upotevu wa samaki hao unapunguzwa kwa kiasi kikubwa.

Dkt.Kimirei ametolea mfano wa moja ya mitambo ya uzalishaji barafu iliyowekwa katika mwambao wa Ziwa Tanganyika lakini wavuvi wakafikiri barafu zinaharibu samaki na hawakutaka kuutumia, lakini wavuvi hao walipokuja kugundua faida ya barafu hivi sasa mahitaji ya barafu hayatoshi.