December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chande aanza kazi akitaka ubunifu Shirika la Posta

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

POSTAMASTA Mkuu Maharage Chande amewasili rasmi Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania leo na kukutana na Menejiment ya Shirika huku akiwaasa Posta kuwa na weledi na kuongeza ubunifu katika utendaji, lengo ikiwa kuongeza tija na kuwahudumia wananchi kulingana na mahitaji yao hususani katika kipindi hiki cha maendeleo ya teknolojia.

Ameyasema hayo wakati wa makabidhiano rasmi ya ofisi na aliyekuwa Postamasta Mkuu  Macrice Mbodo.  Maharage aliteuliwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Postamasta Mkuu wa Shirika tarehe 25 Septemba, 2023.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Maharage amesisitiza uwepo wa ushirikiano baina ya wafanyakazi na kuwa wawazi katika kutekeleza majukumu yao ili kuboresha huduma za Posta kwa manufaa ya wananchi

“Muwe wawazi pale mnapoona kuna mahali pa kushauri msisite kunishauri, ili tuipeleke Posta yetu mbele na nyie muwe wabunifu ili tusaidiane kwenda kidijitali”. Amesema Maharage

Kwa upande wake aliyekuwa Postamasta Mkuu Macrice Mbodo aliiasa Menejimenti ya Shirika la Posta Tanzania kumpa ushirikiano Postamasta Mkuu mteule katika kuendelea kufanya mageuzi ndani ya Shirika.

Katika hatua nyingine Mbodo amewashukuru wafanyakazi wa Shirika hilo kwa ushirikiano mkubwa waliomuonesha kipindi alichokuwa Postamasta Mkuu hadi kupelekea Shirika kupiga hatua kidijitali.

“Ukiona mtu anauwezo wa kuona mbali, usikimbilie kusema huyo mtu ni mrefu, mtazame vizuri anaweza kuwa amesimama juu ya mabega ya wengine, mliamua kukubali nisimame juu ya mabega yenu ili nionekane mimi, ila kazi kubwa inayoonekana sasa ni kwa juhudi zenu, asanteni sana Posta”.