Na Penina Malundo ,Timesmajira
CHAMA cha Mtindo Maalum wa Uzungumzaji Tanzania (CHAMMUTA) kinatarajia kuanza kambi maalum ya Watoto wenye kigugumizi itakayofanyika Dar es Salaam lengo likiwa ni kuwahudumia watoto na vijana kuzungumza kwa kujiamini.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa kambi hiyo, Dudley Mbowe wakati akiongea na waandishi wa habari amesema watoto wenye kigugumizi wanahitaji mazoezi ya kuzungumza kwa kujiamini, ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wanasaikolojia na wataalamu wa mawasiliano na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa kuielimisha jamii kuhusu kigugumizi.
Amesema kambi hiyo inatarajiwa kuanza Juni 23 hadi 27 mwaka huu na kupokea watoto kati ya 30 na 50 wenye kigugumizi ambao watapatiwa mafunzo hayo.
Mbowe amesema kambi hiyo inaenda kaulimbiu ya ‘’Ota, zungumza, ishi’’ inayolenga kuwahamasisha watoto na vijana kufikia ndoto zao kwa kuzungumza kwa ujasiri na kuishi maisha kamili bila woga wala aibu.

‘’Tunaamini kuwa kila mtoto au mtu ana haki ya kusikilizwa, kueleweka, na kuheshimiwa bila kujali changamoto yake ya maisha ikiwemo kigugumizi,’’amesema
‘’Kambi hii itakuwa nafasi ya kipekee ya kuondoa unyanyapaa na kuwawezesha watoto kuota maisha bora si tu kwa kujieleza bali pia kuwa mabalozi wa kuelimisha wengine,’”amesema
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa chama hicho, Ally Baharoon amesema malengo ya chama chao ni pamoja na kukuza ujumuishaji zaidi wenye kigugumizi,ujenzi wa ujasiri na kuelimisha jamii kuhusiana na kigugumizi.
Amesema jamii inapaswa kutambua kuwa neno kigugumizi hakipaswi kutumiwa kama mtu kushindwa jambo fulani kama watu wengi wanavyolitumia katika jamii.

“Ifikie mahali mtu mwenye kigugumizi achukuliwe kama mtu mwingine na neno kigugumizi kisitumike katika kuonekana kama mtu huyu ameshindwa kitu fulani.
“Nayaomba mashirika ya kijamii, sekta ya afya na elimu, sekta binafsi, wahisani, wazazi na walkezi wa watoto wenye kigugumizi kushiriki katika kambi hiyo ambayo italeta mabadiliko chanya kwa watoto, vijana na watu wote sambamba na kuwajengea hali ya kujiamini na kuwa sehemu ya jamii inayoelewa, kukubali na kusaidia maendeleo ya watu,amesema.
Amesema kufanyika kwa kambi huu ni mara ya pili ambapo awali ilianza Zanzibar na kufanikiwa kuwafikia watoto 15 ambao waliwajengea uwezo wa kujiamini .

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani