November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chama Cha Mapinduzi kata ya Ipwani chashinda baada ya wagombea wa vyama vingine kujitoa

Na Esther Macha, Timesmajira,Online ,Mbarali

MSIMAMIZI  wa Uchaguzi Jimbo la Mbarali ,Missana Kwangura amemtangaza  ,Furaha  Chalamila wa chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Diwani Mteule wa Kata ya Ipwani mara baada ya wenzake waliochukua fomu kujitoa kwenye uchaguzi huo.

Akizungumza wakati wa  kumtangaza Diwani huyo  mkurugenzi wa halmashauri hiyo amesema  kuwa waliochukua fomu za kugombea walikuwa wanne kutoka vyama vya CCM, CCK, UDP Pamoja na ACT-Wazalendo na vyama vilivyorejesha vilikuwa viwili .

Amesema kuwa  chama cha ACT- ilipofika Novembar 16 mwaka huu mgombea wa ACT-Wazalendo alijitoa na kwenda kuapa mahakamani.

“Sheria ya Uchaguzi kifungu cha 45 kifungu kidogo cha 2 kinasema kwamba, endapo mgombea  atabaki mmoja katika Kata, Msimamizi wa Uchaguzi atakubaliana na hiyo hali na atatoa taarifa kwa Tume ya Taifa Uchaguzi Pamoja na kumjulisha mgombea kwa barua kuwa amechaguliwa, ila atatakiwa kutangazwa siku ambayo uchaguzi mdogo unafanyika kwa mujibu wa ratiba.”amesema msimamizi

Aidha amesema  kwa mamlaka aliyopewa kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi chini ya Kanuni ya 60 Kifungu Kidogo cha 2 ya Kanuni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Uchaguzi wa Madiwani mwaka 2020 kumkabidhi hati ya kuchaguliwa kwa mujibu wa kifungu cha 82A cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa sura ya 292 .

Hata hivyo alisema Furaha  Chalamila wa Chama cha Mapinduzi amechaguliwa kuwa Diwani wa kata ya Ipwani Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani .

Akiongea mara baada ya kukabidhiwa hati ya kuteuliwa kuwa Diwani wa Kata ya Ipwani , Furaha  Chalamila ameshukuru kwa kuchaguliwa kuwa diwani na ameahidi kuwawakilisha vyema wananchi wa kata ya Ipwani kwenye baraza la Madiwani ili kuweza kutatua changamoto zote zinazowakabiri kwa wakati.

“Nakishukuru chama changu cha CCM kwa kuniamini, hawakukosea kunichagua, nitafanya bega kwa bega kupitia Sera na Ilani ya CCM kwa kushirikiana na wananchi kutatua changamoto nyingi zilizopo zikiwemo za barabara, maji, Afya, Umeme, na ninawaahidi sita waangusha.” ameseema  Chalamila

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mbarali , Clemence  Mponzi amesema kuwa amefarijika sana kupata Diwani Mwingine wa CCM mara baada ya aliyekuwepo kutangulia Mbele za haki, na anajua kuwa diwani Mpya atatekeleza ilani kwa yale mambo yaliyoachwa na Mwenzake na amemtaka kufuta makundi na kushirikiana na wenzake waliokuwa kwenye kinyang’anyiro na kwa yale yatakayomtatiza asisite kumtafuta ili washirikiane kuyatatua.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria kutangazwa kwa Diwani wao akiwemo Ndugu Exaudi Kapalila na Bi Graciana Njwilu walisema kuwa wamepata kero nyingi sana tangu Diwani wao kufariki kwani walikosa mwakilishi kwenye baraza la madiwani sambamba na kukosa mtu wa kupeleka kero zao ili wazifikishe kwa viongozi wakubwa.

Hata hivyo wameomba diwani huyo mpya kuanzia pale alipoishia mtangulizi wake hasa katika masuala ya Afya na Elimu na kuahidi kumpa ushirikiano.

Furaha Chalamila, amechukua nafasi hiyo mara baada ya aliekuwa Diwani wa kata hiyo Mahamud Banichuma Mlwale kufariki dunia Agosti 28.