November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chalamila awatoa hofu wawekezaji suala la umeme



Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewahakikishia wafanyabiashara na wenye viwanda kuwa tatizo la kukatika kwa umeme litaisha hivi karibuni kutokana na mikakati kabambe iliyofanywa na Serikali ikiwemo kutafuta vyanzo vipya vya nishati hiyo.

Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mkutano baina yake na wanachama wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI).

Amesema anafahamu changamoto kubwa ya umeme ambayo wafanyabiashara hao wanapitia kutokana na kukatika mara kwa mara lakini serikali imesimama imara kuweka mipango ambayo itaondoa hali hiyo kwa muda mrefu.

Amesema ukame uliopita ulipunguza kiwango cha maji hivyo kupunguza uzalishaji wa umeme unaozalishwa kwa njia ya  maji na kuongeza kuwa sababu nyingine ya kupungua kwa umeme ni ongezeko la watumiaji wa nishati hiyo.

“Watumiaji wa umeme wamekuwa wengi lakini umeme ni ulele ndiyo maana serikali inafanya jitihada kupata vyanzo vingi vya umeme na kuna bwawa la Mwalimu Nyerere Rufiji utakaozalisha Megawati 2115, kuna mradi wa Rusumo kwa hiyo ndani ya muda mfupi ujao hali itakuwa nzuri,” amesema   

Kadhalika, Chalamila amesema Mkoa wa Dar  Salaam kwa sasa hauna shida ya maji kwani wakati mahitaji ya kila siku ni lita milioni 544 lakini uzalishaji wa maji ni lita milioni 590  hivyo kuwa na ziada ya uzalishaji.

Amesema tatizo lililopo ni kasi ya Mamlaka husika kuunganisha wananchi na huduma hiyo na kuongea kuwa baada ya ukame wa mwaka jana serikali iliamua kuingilia kati kwa kuchimba visima.

Amesema jumla ya visima tisa vilichimbwa kukabiliana na hali hiyo na mpaka sasa visima sita vinafanyakazi na tayari tenki lenye uwezo wa kubeba lita 6,000,000 limeshajengwa kuondokana na adha ya maji.

“Upande wa maji kilichobaki ni kuharakisha mtandao wa maji uwafikie wananchi wengi na jambo lingine ambalo Rais amelifanya ni kuwekeza kwenye bwawa la Kidunda ambalo litaleta maji Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani lakini nanyinyi kwenye shughuli zenu muwe mnafikiria suala la mazingira kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi,” amesema

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa  Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI), Leodegar Tenga, ameiomba serikali kupunguza utitiri wa tozo za magari ya wafanyabaishara kuingiza bidhaa katikati ya mji kwani zinaongeza gharama za uzalishaji.

Amesema wenye viwanda wanatengeneza bidhaa ambazo wanalazimika kuzisambaza maeneo ya mijini lakini ili magari yao yafiki mjini yanalazimika kutoa tozo zinazoanzia 20,000 kwa magari madogo, magari  ya ukubwa wa kati 50,000 kwa siku au 200,000 kwa mwezi.

 “Hii inasikitisha sana mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kasababu hakuna mtu anayeweza kuzalisha bidhaa asizipeleke mjini lakini anapozipeleka anaadhibiwa kwa kutozwa msururu wa tozo kwa hiyo tunaomba serikali iliangalie maana ni kilio cha muda mrefu,” amesema

“Mzalishaji anapotozwa mlundikano wa tozo anaongezewa mzigo mkubwa sana kwenye uzalishaji na tozo hizo zimekuwa zikisababisha usumbufu mkubwa kwa magari yao kukamatwa mara kwa mara na kupelekwa kwenye yadi ambako wanalazimika kulipa fedha nyingi,” amesema

Pia Tenga ameiomba serikali itengeneze mirefeji ya kuchukua maji wakati mvua inaponyesha kwani kwenye maeneo ya Chang’ombe hali imekuwa mbaya wakati wa mvua za masika.

“Barabara zile huwa zinaharibika sana kwasababu hakuna mitaro na msongamano wa magari unakuwa mkubwa sana tunaomba TARURA wafanye jambo kupunguza usumbufu huu,” amesema

Kadhalika, Tenga amesema kwenye maeneo ya viwanda kumezuka bandari kavu (ICD) nyingi hali ambayo imesababisha msongamano mkubwa wa magari mengi makubwa kiasi kwamba wenye viwanda wanakosa fursa ya kufanya shughuli zao.

Amesema magari yanayoingiza kwenye ICDs hizo yamekuwa wakati mwingine yakiziba barabara na kusabbaisha usumbufu mkubwa kwa wenye viwanda.