Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Viongozi wa Serikali na Chama tawala kuwapa ushirikiano viongozi wa vyama pinzani walioshinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwani wameaminiwa na wananchi.
Hayo yamesemwa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA. Amos Makalla kwenye mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo Novemba 29, 2024 katika Ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba jijini ,Dar es Salaam.
CPA. Makalla amesema, kampeni zimeisha hivyo ni vyema viongozi wote wakaungana na kuwaletea maendeleo wananchi, huku akisema kuwa kila kiongozi aliyechaguliwa ametokana na kuaminiwa na wananchi wa sehemu husika.
“Kampeni zimeisha na hivi sasa sisi ni wamoja hivyo nitoe rai kwa viongozi wa Serikali na chama tawala kutoa ushirikiano kwa viongozi wa vyama vyote bila kubagua kwani viongozi wote waliochaguliwa wametokana na imani ya wananchi katika maeneo yao.
Tufanye siasa kwa kushindana kwa hoja lakini linapofika suala la kuwatumikia wananchi tuache mambo mengine pembeni na tujenge nchi yetu”, amesema CPA. Makalla.
Pia CPA. Makalla amesema kuwa, CCM imeshinda kwa kishindo kutokana na maandalizi iliyofanya kwa kipindi chote hadi kufikia kampeni ikiwa pamoja na chama hicho kuzitumia 4r za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kama nyenzo yake kuu.
Amesema, kufuatia matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yaliyotangazwa jana na Waziri, Ofisi ya Rais, Tawara za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohammed Mchengerwa na kukitaja chama hicho kupata ushindi wa Mitaa kwa asilimia 98.8, Vitongoji asilimia 98, Wajumbe wa Vijiji asilimia 99 na Wajumbe wa Mitaa asilimia 99, kumeendelea kuamsha hamasa kubwa kwa chama hicho kuendelea kuwatumikia wananchi kwa weledi.
“Jana tumeshuhudia Waziri Mchengerwa akitangaza matokeo ya uchaguzi na nyie ni mashahidi kwamba matokeo yaliyotangazwa yameipa ushindi CCM wa kishindo, Mitaa asilimia 98.8, vitongoji asilimia 98, wajumbe wa vijiji asilimia 99 na wajumbe wa mtaa asilimia 99.
Hii inamaanisha kuwa tulijiandaa vizuri na kufanya kampeni za kisayansi, lakini wakati sisi tunakibiresha chama kwa kuzunguka Mikoa yote 20 na kusikiliza kero za wananchi, kuangalia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya 2020/2025 wenzetu wao hawakufanya hivyo walikuwa busy na maandamano na wengine kwa takribani ya miezi Saba inasemekana hawakuonekana katika maeneo yao wameenda kipindi cha kampeni ndiyo utegemee chama hicho kishinde kweli? Aliongeza CPA. Makalla kwa kuuliza.
CPA. Makalla Amesema, uchaguzi ulikuwa na hamasa kubwa katika chama na watanzania kwa ujumla, hususani kwenye kujiandikisha katika daftari la makazi, kampeni na kupiga kura, huku akisema kuwa, Serikali za mitaa ni muhimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Sambamba na hayo, amewataka viongozi wote wa CCM waliochaguliwa kwenda kuwajibika kwa wananchi kwa kusoma taarifa za mapato na matumizi na kutoa huduma bora ili kubeba dhamana na imani waliyopewa na wananchi.
“CCM kimepokea ushindi huu kwa furaha akubwa tumekuwa katika kampeni kwa siku saba kuanzia tarehe 20 hadi tarehe 26 na tarehe 27 tukaenda kupiga kura ahadi yetu ilikuwa ni kuongozwa na 4R za Rais Samia,” ameongeza.
Aidha, CPA. Makalla, ametoa sababu zilizoipa ushindi CCM kuwa ni pamoja na wananchi kurishishwa na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020/2025, vyama vya upinzani kutojiandaa na uchaguzi huo ikiwa pamoja na migogoro iliyopo ndani ya vyama hivyo.
” Niseme tu kuwa sababu moja wapo ya CCM kushinda ni pamoja na wananchi kuridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020/2025 na, vyama vya upinzani kutojiandaa na uchaguzi lakini pia nyingine ni migogoro iliyopo ndani ya vyama vyao nyie wenyewe mashahidi kwa Yale yaliyokuwa yanaendelea kule Arusha chama kimoja kuwa na mgogoro wa ndani ya chama chao.
Lakini CCM huwezi kusikia hayo yakitokea ni kwasababu kila siku chama kinatoa mafunzo kwa maafisa wake pamoja na viongozi wa chama na ninashukuru nikiwa kama mlezi wa Dar es Salaam kuona imechukua Mitaa 563 kasoro mmoja ambao umeenda ACT Wazalendo”, amesema CPA. Makalla.
Sambamba na hayo, CPA. Makalla amesema, CCM inalaani vitendo vya kikatiri vilivyojitokeza katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, kufuatia mauaji ya vipigo yaliyofanyika kwa baadhi ya viongozi wa vyama ikiwemo kuuwawa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, Christina Kibiki aliyeuwawa kwa kupigwa bastora na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake.
Pia amesema CCM inawashukuru watanzania wote kwa kuiamini na kuipa ushindi mkubwa na kusema kuwa, viongozi wote wa CCM waliochaguliwa wapo tayari kwenda kuwatumikia wananchi katika kuwaletea maendeleo hususani katika utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2020/2025.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM