January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yataka haki sawa kwenye uchaguzi

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, ametoa msisitizo kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutenda haki kwa vyama vyote vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

Amesema katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, wapo wagombea wa CCM ambao wamewekewa pingamizi, hivyo madai ya vyama vya upinzani kwamba wagombea wao pekee ndiyo waliowekewa pingamizi yanalengo la kuwahadaa Watanzania.

CPA Makalla aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam leo, ambapo amesisitiza CCM ipo tayari kushiriki uchaguzi huo na kitaibuka mshindi kwani kimejiandaa ipasavyo.

“Nitume nafasi hii kuwaomba TAMISEMI ambao ndiyo wasimamizi wa uchaguzi huu, waitendee haki CCM na vyama vingine vyote vitendewe haki. Tunaamini uchaguzi utakuwa huru na haki na atakayeshinda kwa haki, atangazwe.

“CCM hatuhitaji upendeleo, hatuhitaji kubebwa, tuko tayari kwani tulishajipanga. Hatuhitaji mbelekeo na TAMISEMI itende haki kwa vyama vyote vya sisasa vilivyoweka wagombe na sisi tupo tayari kushindana na tutashinda kwa haki,” amesisitiza.