January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yaridhishwa jitihada za Serikali ya Rais Samia

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online,Dar

CHAMA Cha Mapinduzi kimesema kinaridhishwa na kutambua jitihada kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya uwekezaji, ambapo mazingira ya mazuri ya kuaminika na kuvutia ya uwekezaji nchini yamepelekea milango ya uchumi wa nchi kuanza kufunguka kwa kasi.

Jambo hilo linatoa taswira mpya ya Taifa kupiga hatua za kimaendeleo. Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ameyaeleza hayo Makao Makuu ya CCM, jijini Dodoma wakati akizungumza na ujumbe wa Watendaji wa ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji uliongozwa na Prof Godius Kahyarara.

Amesema msisitizo na maelekezo ya CCM kwa Serikali ni kuhakikisha wanaendelea kutengeneza fursa za ajira, kukuza uchumi na kuongeza pato la Taifa kupitia uchumi wa viwanda kama ilivyoelekezwa katika ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025.

“Chama Cha Mapinduzi kinaielekeza Wizara kuendelea kutekeleza mambo yaliyoainishwa katika Ibara 17, 18, 22 mpaka 32 ambapo kwa mwaka 2020 mumeanza vyema kwa kuanza kusajili miradi 169 iliyozalisha ajira 10,000 na kufikia Aprili 2021 miradi 150 imesajiliwa ambapo kiwango cha ajira hakijafikia lengo, hapa tuna kazi ya kufanya na maelekezo ya Chama mkajipange vyema,” amesema Shaka.

Shaka amefahamisha kuwa CCM inaitaka wizara hiyo kuendelea kuhamasisha sekta binafsi kutumia sayansi, teknologia na ubunifu ili kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kufanya uwekezaji hasa katika kufanya utafiti wa teknologia za kisasa.

Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka (kusho) akiwa kwenye mazungumza na ujumbe wa Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji uliongozwa na Prof Godius Kahyarara, uliomtembelea ofisi kwake Makao Makuu ya CCM, jijini Dodoma jana.

“Shirikianeni na wizara ya Fedha kuimarisha huduma za kiuchumi, kifedha na upatikanaji wa mikopo. Lazima muweke mkazo zaidi katika kuwalinda, kuwasimamia wawekezaji walioko chini ili waendelee kukua na kuimarika zaidi na waone nchi yetu ndio sehemu sahihi ya uwekezaji duniani,” alisema Shaka.

Kwa upande wake Prof. Kahyarara alisema namna wizara hiyo ilivyojipanga kutekeleza maelekezo ya chama kupitia ilani uchaguzi ya 2020-2025, pamoja na maelekezo ya Rais Samia ambapo wamepiga hatua kubwa katika kuandaa mazingira mazuri ya uwekezaji sambamba na kukamilisha maandalizi ya kuanza kwa kongano za viwanda (industrial parks) ambapo msukumo wa kipekee umetolewa katika maeneo ya Kibaha, Magu, Manyoni, Kilosa na Mufindi katika awamu ya kwanza.

“Hali ya uwekezaji nchini sio mbaya tumepiga hatua kubwa muda sio mrefu tutawajuilisha Watanzania namna Serikali ya Rais Samia ilivyofanikiwa kwa kiasi kikubwa katika eneo hilo.

Aidha miradi mikubwa miwili ipo mwishoni kuanza uchakataji wa alizeti na uzalishaji wa sukari ambayo itazalisha ajira 325,000 ambazo zitakuwa ni sehemu ya ukombozi mkubwa kwa vijana,” amesema Prof Kahyarara