Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WAKAZI wa kata ya Isevya katika halmashauri ya manispaa Tabora wamepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya wilaya na Mkoa kwa kufuatilia mara kwa mara utekelezaji miradi ya maendeleo ya wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa jana na wakazi wa kata hiyo katika mkutano maalumu wa kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ulioitishwa na diwani wa kata hiyo Ramadhan Kapela ambaye pia ni Mstahiki Meya wa manispaa ya Tabora.
Walisema ufuatiliaji mzuri wa miradi ya maendeleo unaofanywa na viongozi wa chama umepelekea kata hiyo kuwa na maendeleo makubwa ikiwemo miundombinu mizuri ya barabara.
Mzee Seleman Mohamed mkazi wa Mtaa wa Sokoni alisema kata hiyo ilikuwa hoi kimaendeleo lakini sasa inang’ara kutokana na kujengwa barabara za lami katika mitaa mbalimbali na kuwekwa taa za barabarani.
‘Miradi ya sasa inasimamiwa vizuri tofauti na zamani, upigaji ulikuwa mwingi mno, tunawashukuru viongozi wa chama kwa kufuatilia kwa karibu zaidi miradi yote inayotekelezwa katika kata zetu, sasa hivi wizi umepungua’, alisema.
Mkazi wa kata hiyo ambaye pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) katika kata hiyo Asia Mohamed alisema chama kimerejesha heshima ya wananchi kwa kuhakikisha kero zao zote zinatatuliwa.
Alisema utaratibu wa Viongozi wa chama ngazi ya kata, wilaya na mkoa ikiwemo Kamati za Siasa kutembelea miradi ya maendeleo, kuongea na kusikiliza kero za wananchi kumechochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kata hiyo.
Naye Mwenyekiti CCM wa kata hiyo Salum Salehe alibainisha wazi kuwa fedha zote zilizoletwa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya na miundoimbinu ya barabara zimetumika kama zilivyokusudiwa.
Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea kiasi cha sh mil 60 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa na kujivunia shule ya msingi Bombamzinga kuboreshwa na kuwa ya kisasa.
Diwani wa kata hiyo Ramadhani Kapela alisema CCM inajivunia kazi nzuri inayofanywa na serikali yake ambayo imepelekea kata hiyo kuwa na maendeleo makubwa katika sekta zote ikiwemo kuimarishwa kwa ulinzi na usalama.
Alisisitiza kuwa chama kipo karibu sana na wananchi na serikali yake na wanashirikiana kwa kila kitu, jambo ambalo limepelekea fedha zote zinazoletwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo kutumika kama zilivyokusudiwa.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba