January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yapinga kauli ya Nape

Na Agnes Alcardo,Timesmajira Online,Dar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeipinga kauli ya kiongozi wake wa zamani, Nape Nnauye aliyosema, ushindi katika uchaguzi hautokani na wingi wa kura za kwenye boksi, bali unategema nani anayehesabu na kutangaza matokeo.

Nnauye aliyewahi kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, alitoa kauli hiyo jana Julai 15, 2024, usiku alipotembelea soko la Kashai mkoani Kagera na kuzungumza na wananchi.

Katika kuwahakikishia ushindi wa Mbunge wa Bukoba Mjini, Stephen Byabato, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Nnauye ambaye kwa sasa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nnauye alitoa kauli hiyo.

“Unajua nyie sikilizeni, matokeo ya kura sio lazima yawe ya kwenye boksi, inategemea nani anahesabu na kutangaza, kwani kuna mbinu nyingi kuna halali, nusu halali na kuna haramu na zote zinaweza kutumika ilimradi tu mkishamaliza unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe pale nilipokosea!,”alisema Nnauye.

Kauli ya Nape imejibiwa leo Julai 16, 2024 na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPa Amos Makalla, alipozungumza katika mkutano wake wa hadhara katika Uwanja wa Panga uliopo katika Kata ya Kawe, ikiwa mwendelezo wa ziara yake ya siku 10 inayoendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam, huku akidai kuwa, kauli hiyo haitokani na msimamo wa chama hicho kwani yeye ndiyo Mwenezi wa CCM Taifa.

“Kuna kiongozi nimemsikia huko mitandaoni anasema eti ushindi wa uchaguzi hautokani na kura za kwenye boksi, mimi nataka nimwambia hiyo kauli isitazamwe kuwa inatokana na CCM na siyo kweli kwani Mimi ndiyo Mwenezi wa CCM Taifa,”amesema.

Amesisitiza kauli hiyo isitafsiriwe kuwa msimamo wa CCM, badala yake chama hicho kinaheshimu ushindi wa haki katika chaguzi.

Aidha Kwa mujibu wa CPA Makalla, amesema, chama hicho kinaheshimu na kitaendelea kuheshimu matokeo yoyote na uamuzi wowote wa wananchi kupitia sanduku la kura.

“CCM itaheshimu matokeo yoyote na uamuzi wowote wa wananchi kupitia sanduku la kura na yeyote atakayeshinda kwa haki ndiye atakayepewa ushindi,” amesisitiza Makalla.