Na Penina Malundo,Timesmajira
CHAMA cha Mapinduzi( CCM ) ,imeibomoa na kung’oa ngome za wapinzani mkoani Lindi huku kikipokea takribani wanachama 280 wakiwemo viongozi wa upinzani ngazi za juu.
Miongoni mwa viongozi hao wajuu waliohama katika vyama vyao wakiongozwa na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Lindi na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mchinga mwaka 2015,Hamidu Bobali,Mwenyekiti wa Wanawake ACT Wazalendo Lindi Mjini,Hawa Kipara na Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Mchinga,Issa Sapanga.
Pia yupo Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Pwani ambaye amekuja kumsindikiza aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mchinga pamoja na Madiwani mbalimbali na wanachama wa vyama hivyo.
Akizungumza leo mara baada ya kupokelewa ndani ya Chama cha CCM,katika viwanja vya Shule ya Sekondari Mpilipili Mkoani Lindi,Bobali amesema leo anahitimisha miaka 20 ya kuwa nje ya chama cha CCM ambapo katika kipindi cha miaka hiyo, wapinzani waliweza kumuamini na kumpatia nafasi mbalimbali za kuongoza.
“Wale wenzangu waliniamini kwa nafasi mbalimbali ikiwemo Afisa Utafiti Taifa,Afisa Mafunzo taifa , na Mwaka 2015 walinichagua kuwa mbunge wa Jimbo la Mchinga na kuingia Bungeni kuwatumikia wananchi wa mchinga kwa tiketi ya Chama cha Wananchi Cuf,”amesema na kuongeza
“Mwaka huu ACT Wazalendo walinichagua kuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama hicho,”amesema.
Aidha amesema kama kunawanasiasa wa upinzani wagumu waliogoma kuhama chama kipindi cha nyuma ni yeye nilikuwa ila kutokana na utendaji kazi wa Rais Samia kwa kufanya vitu mbalimbali vya maendeleo vimemfanya kuhama chama cha Act Wazalendo na kuhamia CCM rasmi.
“Rais Samia amefanya vitu kwa macho sio kuniita kunishawishi bali nimeona kwa macho maendeleo anayoyafanya ikiwemo fedha za Mazao ya Korosho ambayo leo wakulima wote wa Korosho tunapewa pembejeo bure,”amesema na kuongeza
“Nakumbuka mwaka 2018 niliondolewa ndani ya Bunge na kubebwa na Jeshi la Polisi nikipambana kuhusu fedha za mazao ya korosho , leo wakulima wote tunapewa pembejeo bure bila kutoa shilingi kumi,”amesema.
Pia amesema kingine kilichomshawishi kuhamia CCM ni pamoja na bandari ya Uvuvi ambayo imeanza kujengwa wilayani Kilwa mkoani Lindi ambapo serikali ilikuwa inapoteza mapato mengi kutokana na bandari hiyo.
“Leo Rais Samia ameingia ameanza kujenga bandari hiyo ambayo inathamani ya Bilioni 266 ambayo inajengwa kilwa mkoani Lindi hili ni jambo kubwa sana kwetu,”amesema.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Mchinga, Sapanga amesema amehama na viongozi wenzake kwenda CCM akiwemo mwenyekiti wa wanawake wa Chadema mkoa wa Lindi, kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya CCM.
“Hapa Lindi mpinzani mwenye fujo nilikuwa mimi, sasa nimehamia CCM, hapa Lindi sasa hakuna upinzani. Ninakwenda kufanya kazi na viongozi wa CCM katika kuwaletea wananchi maendeleo,” amesema Sapanga.
Akizungumza baada ya kuwapokea wanachama hao wapya, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Nchimbi amewapongeza kwa uamuzi wao wa kujiunga na chama hicho katika kuwaletea wananchi maendeleo katika Mkoa wa Lindi na Taifa kwa ujumla.
“Niwahakikishe ndugu zangu kwamba tutawapatia ushirikiano wa kutosha katika uendeshaji wa chama chetu,” amesema Dkt Nchimbi kwenye mkutano.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja