November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yampongeza Rais Samia kwa Nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia ongezeko la mishahara na kupandishwa kwa malipo ya mkupuo ya pensheni kwa wastaafu.

Uamuzi huo wa kupandisha mishahara, ikiwa ni pamoja na kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3, ambao umefanyika kwa kuzingatia taratibu za mwenendo wa uchumi, pia ule wa kuelekeza kukamlishwa kwa taratibu za kisheria kuhakikisha malipo ya mkupuo ya wastaafu yanapandishwa kutoka asilimia 25 hadi asilimia 33.

Huu ni mwendelezo wa hatua kadhaa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya CCM awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuboresha maslahi na stahiki za wafanyakazi nchini.

Tayari serikali ilishapunguza kodi ya mapato katika mishahara ya wafanyakazi (PAYE) kutoka asilimia 9 hadi 8, kufuta tozo ya kulinda thamani ya mkopo ya asilimia 6 (Value Retention Fee) kwa wanufaika wa mikopo elimu ya juu wakati wa marejesho na upandishwaji wa madaraja kwa kuzingatia miundo ya utumishi wa kada mbalimbali.

Hatua zote hizi ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 -2025, ibara ya 130, ukurasa wa 180-181.

Aidha nyongeza ya mishahara ni utekelezaji wa ahadiambayo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliitoa kwa wafanyakazi kupitia hotuba yake kwa taifa Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi, 2022), kuwa ‘Jambo lao lipo na linafanyiwa kazi’Utekelezaji wake umedhihirisha jinsi Rais Samia Suluhu Hassan alivyo kiongozi msikivu, anayejali wananchi wake, muungwana wa vitendo na zaidi yuko imara kuhakikisha Serikali ya CCM anayoiongoza, inaendelea kuwa tumaini la watu kwa kugusa maisha yao kwa namna chanya.

Vile vile uamuzi wa nyongeza ya mishahara na malipo ya mafao kwa mkupuo umefikiwa baada ya kuwepo majadiliano yaliyohusisha serikali na wadau wanaohusika vikiwemo vyama vya wafanyakazi kupitia Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

Mchakato huu umeendelea kuthibitishia dunia kwamba uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni shirikishi na wenye uwazi sifa ambazo ndio msingi wa utawala bora.

Chama Cha Mapinduzi kinatoa wito kwa wafanyakazi nchini kuendelea kuiunga mkono serikali, kushikamana, kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na weledi ili kuleta tija zaidi katika maendeleo ya Nchi yetu.