Na Mwandishi wetu, Times Majira Online
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla ameendesha harambee ya kumchangia Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu ili aweze kutengeneza gari lake analolitumia kwenye shughuli zake.
Harambee hiyo imefanyika leo Alhamisi, Agosti 15, 2024, Uwanja wa Furahisha, jijini Mwanza kwenye mkutano wa hadhara ambapo Sh5.3 milioni zimepatikana.
Makalla ameendesha harambee hiyo kwenye mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi kwa kile alichoeleza ni kuguswa na hali ngumu anayopitia kiongozi huyo wa Chadema.
Amesema amesikitishwa na taarifa iliyotolewa na kada wa zamani wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa kwamba wakati kiongozi wake akipaa na chopa angani na msafara wa magari 15, Lissu amekuwa akitumia gari moja bovu na walinzi wake licha ya hali aliyonayo.
“Nimesikitishwa sana na Lissu kuendeshwa kwenye gari bovu. Nimesikitishwa sana, naomba tumchangie, mwenye kuchangia chochote alete hapa.”
“Lissu ni ndugu yangu, natoka naye Singida, yoyote aliyeguswa amchangie Lissu gari lake likatengenezwe. 4R za mama zifanye kazi yake,” amesema Makalla huku baadhi ya makada wa chama hicho akiwemo Katibu Mkuu wakichangia.
Baada ya harambee hiyo iliyoendeshwa kwa dakika 15, zilipatikana Sh5.3 milioni ambazo zitakabidhiwa kwa Lissu ili zimsaidie kutengeneza gari lake analolitumia kwenye ziara mbalimbali za kichama.
Makalla amesema fedha hizo zitawekwa kwenye akaunti ya Lissu moja kwa moja na risiti ya muamala huo atapatiwa muhusika kama ushahidi wa mchango huo wa wanaCCM.
Alipotafutwa kuzungumzia kitendo hicho kilichofanywa na CCM, Lissu amewashukuru CCM kwa mchango na kwamba atazipokea fedha hizo kama ambayo amekuwa akipokea kutoka kwa makundi tofauti ya watu.
“Nawashukuru, kama nilivyosema…hatukusema tunachangiwa na wanaChadema peke yao, kama nilivyotibiwa, sikutibiwa na wanaChadema peke yao. Kwa hiyo, wakichangia nitazipokea, sina sababu ya kukataa,” amesema Lissu.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato