Na Mwandishi Wetu,timesmajira, Kigoma
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM)Taifa, Idara ya itikadi na uenezi CCM Shaka Hamdu Shaka ameufananisha uchaguzi mdogo wa majimbo ya Muhambwe na Buhigwe kama vita vya Kagera vilivyomgaragaza na kumuondoa Nduli Idd Amin Dada na majeshi yake ndani ya mipaka ya Tanzania mwaka 1978/79,ndivyo watakavyowagaragaza wapinzani wao.
Pia amesema, Chama kimeweka mpango katika majimbo kuhakikisha wanashinda kwa haki, amani na kwa ushindani wa kidemokrasia .
Shaka ameeleza hayo jana wilayani Kibondo mkoani Kigoma, wakati wa Uzinduzi wa Mkutano wa hadhara wa Kampeni mbele ya mgeni rasmi Mjumbe wa kamati kuu ya CCM,Majaliwa Kasim Majaliwa.
Amesema CCM ni waumini wa demokrasia shirikishi hivyo wameshaingia kwenye uwanja wa mapambano hawatarudi nyuma hadi ushindi utakapopatikana.
“Ni lazima adui apigwe bila huruma na kuhakikisha majeshi yao yanafukuzwa hadi nje ya karibu na mipaka ya DR Congo, Mwaka 1978 nchi yetu ilivamiwa na Majeshi ya Uganda tukalazimika kuyachakaza,”amesema na kuongeza
“ Kipigo kama kile kitawapata tena watani wetu katika majimbo ya Muhambwe na Buhingwe, kwani sababu ya kuwapiga watani zipo, nia na uwezo wa kuwatandika upo hivyo kazi iliobaki ni moja tu ya kuwashinda kwenye chaguzi zote mbili kwenye majimbo hayo,”amesema
Amesema katika uchaguzi huo watashinda kwa mbinu za matumizi ya sera na sayansi ya siasa hatimaye kuwaacha mbali washindani wao kwani baadhi ya vyama vinashiriki uchaguzi huu kwa lengo la kusindikiza Chama Cha Mapinduzi na wagombea wake.
“Tumebeba baadhi ya mitambo muhimu inayoweza kupiga katika masafa mafupi na marefu,kazi ilio mbele yetu ni kuwatandika bila huruma watani wetu ili kuwafundisha nidhamu ya siasa ,” Amesema
Aidha amesema kwa kufuata katiba ya chama chao kimefanya vikao vyake kuanzia ngazi za chini hadi juu vya chama na kuyapitisha majina ya wagombea walioingia kuwa sifa na walioshiriki kwenye mchakato huo wanaendelea kutoa ushirikiano kwa wenzao.
“CCM si chama cha nongwa au mizengwe au kuwekeana mifundo na vinyongo, Uchaguzi ndani ya chama unapomalizika kila mwanachama hutakiwa kuheshimu maamuzi kwani Jeshi letu ni moja hivyo kila askari hutakiwa kwenda mstari wa mbele ,”ameeleza Shaka
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais