Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
WATAALAMU na Watendaji wa Halmashauri ya Manispaa Tabora wametakiwa kuhakikisha maazimio yote yanayotolewa katika vikao vya baraza la madiwani yanatekelezwa kwa wakati ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora Mjini Mohamed Katete alipokuwa akizungumza na madiwani, wataalamu na watendaji wa kata zote katika kikao cha baraza la madiwani wa manispaa hiyo kilichofanyika jana.
Amesema kuwa madiwani wa kata ndio wawakilishi wa wananchi na agenda zote zinazowasilishwa na kujadiliwa katika vikao hivyo zinawalenga moja kwa moja wananchi hivyo maazimio yoyote yanayotolewa ni kwa manufaa yao.
Amesisitiza kuwa maazimio yanayotolewa yamebeba mstakabili wa ustawi wa jamii katika kata husika ikiwemo kumaliza kero zinazowakabili, sasa kama hoja itatolewa na kuazimiwa lakini isitekelezwe wananchi hawatendewi haki.
‘Wananchi waliwachagua madiwani, wabunge na Rais ili wawaletee maendeleo na vikao vyote vya madiwani vipo kisheria hivyo maazimio yanayotolewa ni lazima yatekelezwa ili wananchi waendelee kuwa na imani na wawakilishi wao’, ameeleza.
Mwenyekiti amepongeza kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya 6 chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kujali ustawi wa wananchi na kuendelea kuleta mabilioni ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Amefafanua kuwa wananchi wana imani kubwa na serikali yao kwa kuwa inawafanyia mambo makubwa, hivyo akatoa wito kwa wataalamu, watendaji na madiwani kuhakikisha fedha zote za miradi ya maendeleo zinasimamiwa ipasavyo.
Amebainisha kuwa CCM inaridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo Eliasi Kayandabila, Mstahiki Meya Ramadhan Kapela na Wataalamu wote ila akawataka kuongeza kasi ya utatuzi kero za wananchi.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Tabora Mjini Daniel Mhinda amebainisha kuwa kuwa chama kinawategemea sana wataalamu na watendaji wa manispaa hiyo kwa kuwa ndiyo wanaotekeleza ilani ya uchaguzi kama ilivyoainishwa na chama.
Amewataka kushirikiana na kushikamana katika kutekeleza shughuli za maendeleo ili wananchi wafurahie kazi nzuri inayofanywa na serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi na kero zao pia zitatuliwe kwa wakati
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba