December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM Tabora wazoa Makada wa CHADEMA, CUF

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tabora Mjini kimeadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa kwake kwa kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kupokea makada 3 na wanachama wengine zaidi ya 21 kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Wananchi (CUF).

Makada waliopokelewa ni Ramadhani Msuka aliyekuwa Mkurugenzi wa Wazee wa Chama cha Wananchi CUF Wilaya ya Tabora Mjini na Mwenyekiti wa chama hicho Kata ya Ipuli katika halmashauri ya manispaa Tabora.Wengine ni Fredrick Ndalawa aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA Kata ya Mtendeni na Kiongozi wa Vijana wa kata hiyo na Feruzi Hussein aliyekuwa Mhamasishaji Mkuu wa CHADEMA, Katibu Kata na Mjumbe wa Kamati ya Elimu wa chama hicho kata ya Ipuli.

Wakizungumza baada ya kurejesha kadi za vyama vyao kwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora, Mohamed Katete na kukabidhiwa kadi mpya za CCM walisema wamechoshwa na ubabaishaji uliojaa ndani ya vyama vyao.

Feruzi Hussein alisema chama chake cha CHADEMA hakijali watu wa chini na hakuna demokrasia ya kweli ndani yake, wanachokisema nje ni tofauti na kinachofanyika ndani.

Alibainisha kuwa utendaji mzuri wa Rais Samia Suluhu Hassan, moyo wake wa upendo, mpenda maendeleo na mtenda haki kwa wananchi wote pasipo kuangalia itikadi zao za kisiasa ndiyo yamemvutia na kuamua kurejea CCM.

‘Rais Samia hana siasa za chuki, ni msikivu, ndiyo maana anapendwa na wapinzani na kila siku wanampongeza kwa nia yake ya kulifanya taifa kuwa kitu kimoja na kuendelea kudumishwa amani, upendo na mshikamano’ alisema.

Ramadhan Msuka kutoka CUF alisema viongozi wa vyama vya upinzani wengi wao sio waadilifu, wamejaa ubabaishaji mtupu, hata wanachama wao sasa wanamwona Rais Samia kuwa mkombozi wa kweli wa demokrasia hapa nchini.

Aliahidi kuwa wamerudi nyumbani kwenye demokrasia ya kweli na wako tayari kushirikiana na wanaCCM wote kujenga nchi yao na kunufaika na yale yote yanayofanywa na serikali ya CCM.

Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo, Mohamed Katete aliwakaribisha nyumbani na kuwataka washirikiane na wanaCCM wote ili kuhakikisha chama chao kinaendelea kuwa mtetezi wa kweli wa wanyonge na kuwaletea maendeleo.

Katibu wa CCM Wilaya, Neema Lunga alisema wanajivunia chama chao kutimiza miaka 46 tangu kuzaliwa na kubainisha kuwa katika maadhimisho hayo wametembelea shule na hospitali na kutoa msaada kwa wagonjwa ikiwemo kupanda miti zaidi 5500.

Aliongeza kuwa wamegawa maboksi 50 ya madaftari kwa shule mbalimbali, wamechangia chupa 50 za damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali na vituo vya afya mbalimbali,

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tabora Mjini Mohamed Katete akiwakabidhi Kadi mpya za CCM Makada 3 kutoka vyama vya CHADEMA na CUF waliowakilisha wanachama wengine zaidi ya 21 kutoka vyama hivyo waliohama vyama vyao na kurejea nyumbani CCM ambapo aliwahakikishia kuwa CCM kitaendelea kuwa mtetezi wa kweli wa wanyonge na kuwaletea maendeleo. Picha na Allan Vicent.