*Ni kwa kupeleka fedha nyingi za maendeleo kwa wananchi, Makalla
ataka kura zote ziende kwake, ataka wananchi wasirudie kuonja sumu
Na Agnes Alcardo, Singida
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Rais Samia Suluhu Hassan, amepeleka fedha nyingi za maendeleo kwa wananchi kuliko awamu zote na kila mmoja anakubaliana na hilo hususani wabunge.
Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo wa CCM , Amos Makalla, akiwa kwenye ziara na Katibu Mkuu CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, mkoani Singida.
“Mafanikio haya tuyaseme wakati wote, hata balozi (Emmanuel Nchimbi) anapaswa kuyasema, kuna wale wanaosema sasa hivi Watanzania wamekuwa machawa, yaani kila kitu wanamtaja Samia..sasa wanataka tumtaje nani?
Hata wao familia zao zinawapongeza na kuwashukuru pale wanapozifanyia mambo mazuri ndiyo maana na sisi tunamshukuru Rais pale anapotufanyia mazuri na ndiyo utamaduni wetu kushukuru.” Amesema Makalla.
Kutokana na utndaji huo mzuri wa Rais Samia, Makalla aliwataadharisha wananchi wa Mkoa wa Singida, kutofanya makosa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuchagua viongozi wasiyofaa na badala yake wachague viongozi sahihi kutoka CCM.
Amesema ni vyema wananchi wa Singida wakajifunza kutokana na makosa, hususani katika kipindi hiki cha kuelekekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kusema kura za ndiyo ziende kwa Rais Dkt. Samia.
“Kuna watu walishafanya makosa wakaonja sumu ikawadhuru na hivi sasa watakuwa wamejifunza hawatarudia tena makosa.
Hivyo niwaombe na nyie kutoka maeneo yote katika mkoa huu msifanye makosa ya kuonja sumu kwa kuchagua viongozi ambao hawapo kwa ajili ya maslahi ya wananchi, isipokuwa kwa manufaa yao wenyewe,” alisema Makalla na kuongeza;
“Chagueni viongozi wenye nia ya dhati ya kuhudumia wananchi kutoka CCM na maendeleo mtaendelea kuyaona.”
Pia alitoa pongezi kwa viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya kuhakikisha wanasimamia Ilani ya CCM katika kuleta maendeleo ya Mkoa wa Singida.
” Shukrani zangu za dhati ni kwenu viongozi wetu wa Chama kutoka ngazi mbalimbali, kwanza kwa umati tunaoukuta maeneo mbalimbali tangu tulipoanza ziara yetu jana mkoani humu ni wazi kuwa CCM Mkoa wa Singida ina mahusiano mazuri na wananchi wake na hii yote ni kutokana na utekelezaji wa Ilani yetu ya chama katika kuwaletea maendeleo wananchi wetu katika maeneo mbalimbali,” amesema.
Aidha, amesema katika ziara hiyo wameridhishwa na taarifa ya chama Mkoa kuwa hali ya kisiasa mkoani humo ipo shwari na hakuna wasiwasi kuhusu ushindani kutoka vyama pinzani na kusema kuwa, wananchi wa Singida wameonesha kuridhishwa na CCM.
” Kwa hii hali tunayoiona na mapokezi mazuri ya wana Singida ni wazi kuwa wapinzani hawana nafasi, hivyo niwaombe viongozi wa chama tuendelee kuimarisha chama na kuendelea kuwatumikia wananchi, kwani ndiyo waliyotuweka hapa tulipo hivyo viongozi wote kutoka ngazi ya Shina, Tawi na Kata tuendelee kuongeza wanachama wapya, “, ameongeza Makalla.
Sanjari na hayo, amewataka viongozi wa CCM mkoani humo kutenga siku na muda wa kusikiliza kero za wananchi wake na si kuwaachia viongozi wa Serikali pekee.
“Niwaombe ndugu zangu viongozi, suala la kusikiliza kero za wananchi ni letu sote na si suala la Serikali pekee, wekeni muda katika ofisi zenu msikilize changamoto za wananchi na zinazoweka kutatuliwa zitatueni zinazohitaji kutatuliwa na viongozi Serikalini muwaelekeze huko”, ameongeza.
Ziara hiyo iliyoanza Mei 29 na kutarajiwa kumalizika Juni 9 inalenga kufanyika mikoa mitano, Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.
More Stories
Tanga kutumia vituo 5405,kupiga kura leo
NMB yatoa msaada wa vifaa Mufindi
Viongozi wa dini Katavi waomba wananchi kujitokeza kupiga kura