November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM Mkoa wa Tanga waingilia kati mgogoro wa Ardhi

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online. Tanga

Chama cha mapinduzi CCM Mkoa Tanga kimeingilia kati mgogoro wa ardhi unaomuhusu Mkazi wa Magaoni Jijini Tanga Mwanaidi Jumaa Kihiro ambaye anadai kuporwa eneo lake la asili lenye ukubwa hekari 60 lililochukuliwa na mamlaka za serikali na kuuzwa kwa watu wengine kinyume na sheria huku chama hicho kikiahidi kugharamia gharama za wakili ili haki ya mama huyo iweze kupatikana.

Pia chama hicho kimesitisha shughuli zote za uuzaji wa viwanja katika eneo hilo pamoja na kuagiza shughuli zote za ujenzi katika eneo hilo kusiamama mara moja mpaka shauri la kesi hiyo litakapokamilika.

Katibu wa CCM Mkoa Tanga Suleiman Mzee Suleiman amesema kuwa chama hicho kitalishughulikia tatizo hilo kama kosa la jinai ili wahusika walioshiriki kwenye mchakato wa uporaji wa eneo hilo waweze kushugjulikiwa kwa mujibu wa sheria.

“Mgogoro huu kweli ni wa muda mrefu na mpaka ulifika kwenye ofisi ya katibu Mkuu wa CCM Taifa na hatimaye akarejesha maelekezo kwamaana chama kisimamie jambo hili chini ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kwamba mgogoro huu unasimamiwa kisheria ili haki ya upande wa mwenye haki ipatikane, “alisisitiza Katibu Suleiman.

Katibu Mzee alikiri kweli eneo hilo kuendelezwa kwa kiasi kikubwa na mara baada ya kupekua nyaraka za mama huyo zinaonyesha kwamba ni kweli mama huyo ni mmiliki halali japo kuwa hakuwa na hati ya kisheria ya kiserikali wala hati ya umiliki bali alikuwa na karatasi zinazoonyesha kwamba eneo hilo ni eneo lao la asili.

“Inaonekana hapa katikati walitokea wajanja wakaenda kujimilikisha eneo hilo kinyume na sheria bila kufuata taratibu na baada ya kujimilikisha eneo hili wao wanaonekana wamechukua fidia serikalini ili kudhulumu haki ya mama huyo na wanawe na hatimaye kujimilikisha wao kwa faida ya familia zao, “

Ameongeza kuwa hili ni kosa la jinai kwakuwa hiki ni chama dola na ni chama kinachosimamia serikali jambo hili tunaondoka nalo kama ni shitaka, kosa la jinai mama huyu tutamtafutia wakili na chama kitamlipa wakili huyu na baada ya kumlipa akaisimamie haki hii kwakila mtu aliyekula haki isiyo yake awajibishwe kwani chama siku zote kinasimamia haki za wanyonge.

Bi Mwanaidi Jumaa Kihiro ambaye anadai ndiye mmiliki halali wa eneo hilo na Mwanaye Amina Kurumbua wamesema eneo hilo ni la kwao la asili na kwamba udanganyifu uliofanywa kwenye eneo hilo ulifanyika wakati mama yao alipopatwa na ugonjwa wa kupooza.

Bi Mwanaidi amesema nyaraka zote za kuthibitisha kuwa eneo hilo ni lake zipo na kwamba baba yake alinunua shamba hilo kisheria na mashahidi wa pande nne wakiwepo pamoja na wauzaji.

Aidha wameomba chama hicho kuwasaidia kupata haki yao ambayo wameihangaikia kwa kipindi kirefu bila mafanikio yeyote.

Kamishna wa Ardhi msaidizi Mkoa wa Tanga Tumaini Gwakisa amesema kinachoendelea hivi sasa ni kupitia eneo hilo na kuthibitisha mipaka ili kubaini kile anachokilalamika mama huyo na mara baada ya kukamilika watarejea kumpa taarifa ya kile walichokibaini.

Mgogoro huo umedumu kwa takribani miaka 15 sasa na kwamba eneo hilo limemilikishwa watu wengine kwajili ya makazi na kujengwa shule.