Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga
Chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Tanga kimepongeza jitihada zinazofanywa na madaktari bingwa kutoka hospitali ya Benjamini Mkapa ya kukutana na wananchi na kutoa huduma za matibabu ya kibingwa ambazo baadhi ya wananchi wasingeweza kuzipata ikiwemo matibabu ya Moyo, Figo, pamoja na kusafisha damu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga amesema huduma hizo ambazo zimetolewa kwa siku 5 kwenye hospotali ya rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo ni sehemu ya jitihada inayofanywa serikali kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma za afya.
Amesema chama hicho kitaendelea kuwatia moyo madaktari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kushughulika na magonjwa ya wananchi ambayo penhine yangekuwa chanzo cha jamii kupoteza maisha kwa kukosa matibabu.
“Tuliona ni vyema sisi kama chama kufika hapa kwajili ya kuwapongeza kuwatia moyo kwa kazi kubwa wanayoifanya tukifahamu kazi hii ya kuwatibu watu ni kazi ya wito na ndio maana hata Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akiongea na madaktari na kuwatia moyo ya kwamba wanachokipata hakilingani na kazi wanazozifanya, “alisema Mwenyekiti Rajab.
Aidha Mwenyekiti Rajab Amesema kuwa Madaktari bingwa wabobezi kutoka hospitali ya Benjamini Mkapa mbali na kutoa huduma hiyo watawaongezea uwezo madaktari bingwa waliopo katika hospitali ya Bombo.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo Juma Ramadhani Juma amesema wamepokea jumla ya wataalamu 12 ambao watawasaidia kwenye huduma mbalimbali ikiwemo mtaalamu wa mishipa ya fahamu ya ubongo, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, daktari bingwa mbobezi wa figo, madaktari bingwa wa magonjwa ya upasuaji pamoja na madaktari bingwa wa watoto.
“Hawa madaktari bingwa wamekuja kutuongezea uzoefu hususani kwa madaktari bingwa ambao tuko nao kwenye hospitali yetu kiukweli wananchi wa Mkoa wa Tanga wameonyesha mwitikio mkubwa sana wamekuja kupata huduma kwa wingi kila siku kwaniaba ya hospitali ya Bombi tunamshukuru Mheshimiwa Ummy mwalimu mbunge wetu na waziri wa afya kwa kutuletea wataalamu hawa, “alisema Juma.
Naye Daktari wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu Dkt Henry Humba ambaye pia ni Mkurugenzi msaidizi katika Hospitali ya Benjamini Mkapa amesema kuwa mpaka sasa wamepokea wagonjwa wengi wenye matatizo ya macho ambapo takribani watu 194 ambao kati yao 19 wamebainika kuwa na matatizo yanayohitaji upasuaji.
“Kusema ukweli mwitikio umekuwa mkubwa wengine waliokuja kwa wingi ni wenye matatizo ya mifupa na viungo mpaka jana takribani wagonjwa 64 na katika hao wagonjwa 15 wanahitaji kubadilishiwa viungo kama nyonga na magoti na pia wagonjwa wenye matatizo ya ubongo na kichwa tumepokea wagonjwa 25 na katika hao tumepata wagonjwa 3 ambao tayari yumeshawafanyia upasuaji, “alisisitiza Daktari bingwa huyo.
Baadhi ya wananchi Mkoani Tanga waliopatiwa huduma ya matibabu wamesema huduma hiyo imekuja kwa wakati muafaka na kwamba wengi walishindwa kufuata madaktari hao kutokana na kutokuwa na gharama za matibabu.
Huduma hiyo mpaka sasa imewezesha kuhudumia wagonjwa zaidi ya 400 tofauti na matarajio ya kuhudumia wagonjwa 200 ambao walitarajiwa kupatiwa huduma ndani ya muda wa siku 5.
More Stories
Serikali ya Kijiji Ilungu yawakatia bima za afya wananchi 1500
TMA kuendelea kufuatilia mifumo yake
Wassira:Waliopora ardhi za vijiji warudishe kwa wananchi