Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
CHAMA cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mbeya, Chini ya Mwenyekiti wake Patrick Mwalunenge, kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili ya Jijini Dar es Salaam, kimeandaa siku nne zitakazo tumika kutoa huduma ya kimatibabu kwa watu wenye magonjwa ya fahamu.
CCM Mkoa wa Mbeya imeratibu zoezi hilo la kuwaleta madaktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, watakao anza kutoa huduma hiyo Aprili 8 hadi 11, Mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema jana Aprili 2, Mwaka huu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Mkoa wa Mbeya, Christopher Uhagile, amesema, matibabu hayo yatatolewa kwa watu wote wanaosumbuliwa na magonjwa ya mfumo wa fahamu wa Mkoani Mbeya kwa gharama nafuu huku wasiyo na uwezo wa kifedha kupatiwa matibabu hayo bure.
Amesema, dhamira ya CCM ni kutekeleza Ilani yake kama inavyosema ikiwa pamoja na uboreshaji wa huduma ya afya, ambapo amesema, wagonjwa wasiyo na uwezo chama cha CCM chini ya Mwenyekiti wake Mwalunenge, kitagharamia matibabu kwa wagonjwa wasiyo na uwezo wa kifedha.
“Chama cha CCM Mkoa wa Mbeya kama mnavyojua chini ya Mwenyekiti wake Patrick Mwalunenge, kwa kushirikiana na Madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, kinaendelea kuwahudumia wananchi wake wa Mkoa wa Mbeya.
Na sasa chama chetu Mkoa wa Mbeya kimeona ni vyema kilete madaktari bingwa kutoka Muhimbili kwa ajili ya kutoa matibabu kwa watu wenye magonjwa ya mfumo wa fahamu, wagonjwa kutoka pande zote za Mkoa wa Mbeya mnakaribishwa kuanzia tarehe 8 na gharama ni nafuu, kwa wale wasiyo na uwezo wa kifedha mtapata matibabu bure baada ya kufika katika ofisi zetu za chama za hapa mkoani kwa ajili ya kujiridhisha”, amesema Uhagile.
Aidha, amesema kuwa, Mwenyekiti huyo wa CCM Mwalunenge, atahakikisha wagonjwa wote waliofika kwa ajili ya matibabu wanapata matibabu na endapo muda wa siku nne utakuwa mdogo ataongeza siku na kugharamia nahitaji yote ya wagonjwa hao.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi