March 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM Mara wasajili kadi 645,000 za Kielektroniki kuanza kugawa Machi 29,2025

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara

KATIBU wa Siasa,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara Simon Rubugu amesema kuwa, Chama hicho kimepokea kadi za wanachama wa Mkoa huo waliosajiliwa kwa mfumo wa  Kielektroniki zipatazo  645,000, ambapo kinatarajia kuanza zoezi la ugawaji wa kadi hizo  Machi 29, 2025, Mkoani humo.

Rubugu ameyasema hayo leo Machi 27,  2025, wakati akizungumza na Majira Online  Makao makuu ya chama hicho Mjini Musoma na kusema kuwa,kadi hizo zimebooreshwa kisasa  huku akitoa msisitizo kwa Wanachama wa CCM ambao bado hawajasaliliwa kujisajili kwani zoezi hilo ni endelevu.

Amesema,idadi ya kadi hizo  ni zaidi ya asilimia 51 ya makisio ya Wapiga kura na zitasaidia kuwatambua wanachama wa Chama cha mapinduzi kuanzia ngazi ya matawi, Kata, Wilaya hadi Mkoa kabla ya kuingia katika uchaguzi  unaotarajia kufanyika mwaka huu.

“Kadi hizi zitakuwa na faida kwa wanachama ikiwemo kuwatambua wanachama wote kwenye mfumo, urahisi wa kufanya nao mawasiliano, Mwanachama kuitumia kadi  katika matumizi ya miamala, naomba wanachama wakati wanakwenda kuchukua kadi zao waende  na Vitambulisho vyao vya NIDA au Kadi ya Mpiga kura kwa ajili ya kuingizwa kwenye mfumo.”amesema na kuongeza kuwa

“Tunashukuru sana juhudi thabiti zilizofanywa na Mwenyekiti wetu Taifa Ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wanachama wanakuwa kwenye mfumo,  haya ni mageuzi makubwa na mazuri sana kwa chama chetu .” amesema Rubugu. 

Pia, amepongeza miradi ya maendeleo iliyofanywa na  Serikali ya Chama Cha mapinduzi chini ya Rais Dkt.  Samia Suluhu  Hassan ikiwemo ujenzi wa miradi ya Kimkakati kama uwanja wa Ndege wa Musoma, Daraja la Magufuli  Mwanza, Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere,  miradi mbalimbali ya elimu, afya, barabara, maji ambayo amesema itakipa ushindi wa kishindo Chama hicho kwenye uchaguzi Mkuu mwaka huu. 

“Miradi ambayo imefanywa na Serikali uhakika ni kwamba chama  kitashinda  kwa ushindi mkubwa sana, hii ndio reforms ya maendeleo, miradi inaonekana kwa macho.  Mkoa wa Mara tunao uwanja wa Ndege ambao utafungua fursa ya uchumi.Tunao mradi mkubwa wa maji wa Mugango-Kiabakari- Butiama huu umesaidia Wananchi wengi na mradi mwingine wa Maji  upo wa  Rorya unakwenda mpaka Tarime wa Bil. 134, Wananchi wamekoshwa na miradi hii.”amesema.

Aidha, amewataka wanachama wa Chama hicho Mkoa wa Mara kuendelea kushikamana, kupendana na kuachana na makundi madogo madogo. Na pia, waendelee kuyasema kwa Wananchi mema na maendeleo yote ambayo serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inayafanya maeneo mbalimbali hapa nchini