November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yaendelea kujizolea wanachama wa CHADEMA

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeendelea kujizolea Wanachama wapya kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakidai kuwa wamepoteza imani na chama chao na kudai kuwa CCM ndiyo mkombozi wao.

Wanachama zaidi ya watano, kwa mara nyingine tena leo Julai 14, 2024 kupitia mkutano wa hadhara wa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mfunzo CCM Taifa, CPA, Amos Makalla, uliofanyika katika Jimbo la Kibamba Wilaya ya Ubungo, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya simu 10 katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Wanachama hao wameomba kujiunga na Chama Cha CCM kwa kupatiwa kadi na kuwa Wanachama wapya na kurudisha kadi zao za CHADEMA.

Akikabidhi kadi kwa Wanachama hao, CPA Makalla amesema, CCM ndiyo chama kilichopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi wake na kudai kuwa ni wajibu wa Serikali na Chama hicho kuhakikisha inawajali wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo, ikiwa pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zao na si kuzikimbia.

Aidha amewaomba wananchi kuendelea kukiamini chama hicho kwa kukipatia kura nyingi katika chaguzi zijazo kwa kuanza na Chaguzi za Serikali za Mitaa zinazotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu, huku akiwaomba wana Ubungo kukupatia kura CCM katika Mitaa yote 90.

Pia amesema kuwa, kati ya majimbo yaliyokuwa na changamoto kubwa katika upande wa miundombinu ya barabara na majini ni pamoja na Jimbo la Kibamba, ambapo amezitaka mamraka husika kufuatilia na kuzipatia ufumbuzi mapema iwezekanavyo.

Hata hivyo, CPA Makalla amesema, wanachama wanaoendelea kuvihama vyama vyao ikiwemo CHADEMA na kuhamia CCM ni majasiri na ni watu wanaopenda maendeleo, kwani wamechoshwa na siasa zenye maslahi ya watu wachache.

Mmoja wa Wanachama wa CHADEMA aliyehakia CCM leo, ambaye hakutaka jina lake kutolewa kwenye vyombo vya habari, amesema “kiukweli kwa Mambo anayofanya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan nimewiwa kumuunga kono na kuunga mkoni juhudi za Chama cha CCM na Serikali yake kwa ujumla, mana kule kwetu (CHADEMA) tumepoteza muelekeo na CCM ndo Mpango mzima. Amesema Mama huyo.