Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
VYOMBO 11 vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO’s) vilivyopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga vimepewa kompyuta 11 na simu 11 vyenye thamani ya sh. milioni 22.5 kwa ajili ya kutoa huduma kwa wateja wao.
Kompyuta hizo zimetolewa na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Korogwe ikiwa ni mikakati ya kuhakikisha vyombo hivyo pia vinakusanya mapato kupitia Mfumo wa Kielektroniki (Maji IS Billing System) wa utoaji ankara za maji na ukusanyaji wa mapato (Maji IS na GePG).
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi kompyuta hizo Juni 18, 2024 kwa niaba ya Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa, Mhandisi Joyce Malekela amesema kompyuta na simu hizo zilizotolewa kwa CBWSO 11 za Wilaya ya Korogwe ni sehemu ya vitendea kazi kwa ajili ya kufanya kazi ya kukusanya mapato kidijitali zaidi pamoja na kutunza kumbukumbu mbalimbali.
“Tumetoa vitendea kazi hivi kwa lengo la kuweza kuvitumia kwa ajili ya kuweka taarifa zote ikiwemo kujua idadi ya wateja, huduma za maji zinazotolewa na namna ya kutunza kumbukumbu za malipo, Lakini pia kompyuta na simu hizo watakwenda kuzitumia kwenye mafunzo Lushoto kwa ajili ya kuunganisha CBWSO’ kwenye Mfumo wa Kielektroniki (Maji IS Billing System) wa utoaji ankara za maji na ukusanyaji wa mapato (Maji IS na GePG).
“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Pia tunamshukuru Waziri wa Maji Jumaa Aweso kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maji, na kuhakikisha inatekelezwa kwa ukamilifu, na kwa wakati” amesema Mhandisi Malekela.
Kwa upande wake Mariam Kennedy ambaye ni Mhasibu wa CBWSO ya Hale ametoa shukrani kwa Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi Tupa kwani wao ndiyo wamewezesha kupata vitendea kazi hivyo kwa wakati na kuweza kurahisisha shughuli zao.
Naye Raphael Mwajombe ambaye ni Msimamizi wa CBWSO inayohudumia kata za Mashewa, Kizara, Folofolo na Kalalani (MAKIFOKA) ameahidi kuvitunza vitendea kazi hivyo, kwani ni muhimu kwa majukumu yao ya kila siku kwa ajili ya kuchukua kumbukumbu, kuziweka na kuzituma kunako husika.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapatoÂ